Umoja wa Mataifa: Watu 230,000 wamekimbia ghasia mashariki mwa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121616-umoja_wa_mataifa_watu_230_000_wamekimbia_ghasia_mashariki_mwa_drc
Umoja wa Mataifa umesema kuwa, watu wapatao 230,000 wamekimbia ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu kuanza mwaka huu wa 2025.
(last modified 2025-01-18T23:09:49+00:00 )
Jan 18, 2025 23:09 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Watu 230,000 wamekimbia ghasia mashariki mwa DRC

Umoja wa Mataifa umesema kuwa, watu wapatao 230,000 wamekimbia ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu kuanza mwaka huu wa 2025.

Eujin Byun, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, kuongezeka kwa mapigano kati ya jeshi la DRC na makundi yenye silaha katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini, kunachochea moja ya majanga ya kibinadamu ya kutisha zaidi duniani lakini ambayo hayaangaziwi ipasavyo.

Msemaji huyo wa  UNHCR  ameongeza kuwa, mgogoro huo unajumuisha vitendo mbalimbali vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kuwalazimisha watu wengi kuyahama makazi yao. Byun alidokeza kuwa majimbo mawili ya Kivu kaskazini na Kusini tayari yana watu milioni 4.6 waliokimbia makazi yao, na hivyo kuifanya DRC kuwa mojawapo ya nchi duniani yenye wakimbizi wa ndani.

Kundi la waasi la M23 hivi karibuni lilizidisha mashambulizi yake mashariki mwa DRC na kuteka miji muhimu kama Katale na Masisi na kuwalazimisha watu wengi kukimbia makazi yao. Kuna makumi ya makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao mashariki mwa Kongo, lakini waasi wa M23 ambao Kinshasa inasema ni wa kabila la Kitutsi linaloungwa mkono na Rwanda, ndilo kundi maarufu zaidi la waasi.

Serikali ya DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, lakini Rais wa Rwanda, Paul Kagame amekuwa akikanusha mara kwa mara.