Ripoti: Mzozo wa Sudan unazidi kuwa mbaya zaidi
Kamishna wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk amesema kuwa, mzozo wa kivita unaoendelea nchini Sudan unazidi kuwa mbaya zaidi kwa raia.
Turk ameelezea ripoti zinazoonyesha kwamba, makumi ya watu wameuawa katika mashambulizi ya kikabila yaliyolengwa katika jimbo la kusini-mashariki la al-Jazirah na mji mkuu wa Khartoum ambapo vikosi vya kijeshi vya serikali na wanamgambo wa RSF vinapambana kuchukua udhibiti.
Mapigano kati ya Wanajeshi wa Sudan (SAF), wakiongozwa na Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), vilivyo chini ya Mohamed Hamdan Daglo, yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika wiki za hivi karibuni. Türk amesema.
Wakati huo huo, Mkuu wa jeshi la Sudan ameunda kamati ya kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa wakati jeshi lake lililpoukomboa mji wa Wad Madani kutoka kwa wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF).
Wakati huo huo, Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Clementine Nkweta-Salami, ameelezea wasiwasi wake kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mali ambao umesababisha watu wengi zaidi kukimbia makazi yao.
Tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari, Jeshi la Sudan SAF lilianzisha operesheni kubwa ya ardhini ili kurejesha udhibiti wa Wad Madani ambao uko umbali wa takriban kilomita 189 kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Sudan imekuwa katika mgogoro mbaya wa vita vya uchu wa madaraka bainaya makundi mawili ya SAF na RSF tangu katikati ya Aprili 2023. Makadirio ya karibuni kabisa ya mashirika ya kimataifa yanasema kuwa, watu 29,683 wameshauawa tangu wakati huo na milioni 15 wengine wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.