Watu 86 waaga dunia katika mlipuko wa lori la mafuta Nigeria
Watuu wasiopungua 86 wameaga dunia katika Jimbo la Niger, nchini Nigeria katika tukio la mlipuko mkubwa wa lori la mafuta.
Tukio hili lilitokea kwenye barabara inayounganisha mji wa Kaduna na mji mkuu Abuja. Kwa mara nyingine tena, mlipuko huo ulisababishwa na ajali ya lori la mafuta.
Kulingana na Idara ya Usalama Barabarani nchini Nigeria, gari lililokuwa na lita 60,000 za petroli lilipinduka kwenye 'makutano ya Dikko' kati ya Abuja na Kaduna.
Mafuta yaliyokuwa katika tanki yalimwagika chini na kwa mujibu wa Gazeti la kila siku la Nigeria la The Guardian, ambalo linanukuu idara ya Usimamizi wa Dharura wa Jimbo la Niger, ni wakati wa kujaribu kuhamisha petroli kwenye lori jingine la mafuta ndipo mlipuko ulipotokea.
Hii ni ajali ya pili ya aina hii ndani ya miezi mitatu iliyopita. Mnamo Oktoba mwaka jana, matukio kama hayo yalitokea katika Jimbo la Jigawa kaskazini mwa nchi, na kuua zaidi ya watu 170.
Mwanzoni mwa mwezi Septemba pia, makumi ya watu walipoteza maisha baada ya lori la mafuta kuripuka kaskazini mwa Nigeria.
Limekuwa jambo la kawaida huko Nigeria ambapo watu wengi huhatarisha maisha yao kwa kukimbilia malori yanayopinduka ili kuchota mafuta hasa ukizingatia kupanda kwa bei ya mafuta nchini tangu serikali ilipositisha mpango wake wenye gharama kubwa wa kufadhili ruzuku ya gesi.