Rais Tshisekedi akataa mazungumzo ya moja kwa moja na M23
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121650-rais_tshisekedi_akataa_mazungumzo_ya_moja_kwa_moja_na_m23
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amefutilia mbali uwezekano wa serikali yake kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na kundi la M23, akisema kwamba hatua hiyo italipa uhalali kundi hilo.
(last modified 2025-01-19T23:18:57+00:00 )
Jan 19, 2025 23:18 UTC
  • Rais Tshisekedi akataa mazungumzo ya moja kwa moja na M23

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amefutilia mbali uwezekano wa serikali yake kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na kundi la M23, akisema kwamba hatua hiyo italipa uhalali kundi hilo.

Msimamo huo wa Rais Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo uumetangazwa baada ya mkutano uliotarajiwa  kufanyika tarehe 15 Disemba mwaka jana nchini Angola kati ya Rais shisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame kufutwa baada ya pande hizo mbili kushindwa kufikia makubaliano kuhusu masharti ya mazungumzo hayo.

Tshisekedi aliwaambia wanadiplomasia mjini Kinshasa kwamba mazungumzo hayo yameshindwa kwa sababu ya ujumbe wa Rwanda kutoa sharti jipya la kutaka yafanyike mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kundi la waasi la M23.

Hivi majuzi kuulitolewa mwito wa kuanzishwa tena mazungumzo katika ngazi ya juu kati ya DRC na Rwanda. Lakini Rais Tshisekedi amesema kuwa, nchi yake haitakubali kile alichokitaja kama "mashinikizo kutoka nje" kuweka masharti ambayo yanakiuka kanuni na mamlaka ya kujitawala Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kundi la waasi la M23 hivi karibuni lilizidisha mashambulizi yake mashariki mwa DRC na kuteka miji muhimu kama Katale na Masisi na kuwalazimisha watu wengi kukimbia makazi yao. Kuna makumi ya makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao mashariki mwa Kongo, lakini waasi wa M23 ambao Kinshasa inasema ni wa kabila la Kitutsi linaloungwa mkono na Rwanda, ndilo kundi maarufu zaidi la waasi.

Serikali ya DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, lakini Rais wa Rwanda, Paul Kagame amekuwa akikanusha mara kwa mara.