Kenya yatuma wanajeshi zaidi nchini Haiti
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121652-kenya_yatuma_wanajeshi_zaidi_nchini_haiti
Kenya imetuma maafisa 217 zaidi wa polisi nchini Haiti, kama sehemu ya jeshi la kimataifa la kukabiliana na ghasia za magenge katika taifa hilo la Karibia.
(last modified 2025-01-19T23:19:23+00:00 )
Jan 19, 2025 23:19 UTC
  • Kenya yatuma wanajeshi zaidi nchini Haiti

Kenya imetuma maafisa 217 zaidi wa polisi nchini Haiti, kama sehemu ya jeshi la kimataifa la kukabiliana na ghasia za magenge katika taifa hilo la Karibia.

Kulingana na waziri wa mambo ya ndani, Kipchumba Murkomen, maafisa hao waliondoka Kenya siku ya Ijumaa. Murkomen ameongeza kuwa misheni hiyo inayoongozwa na Kenya imepiga hatua kubwa katika kupunguza vurugu za magenge, na kupata sifa kote ulimwenguni, na kwamba ahadi ya kujitolea kwa taifa hilo la Afrika Mashariki haiyumbishwi.

Kenya ilituma wanajeshi wake Haiti kwa mara ya kwanza mwezi Juni na kufikia sasa imetuma zaidi ya wanajeshi 600. Rais William Ruto aliahidi kupeleka wanajeshi 1,000 kama sehemu ya kikosi kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Haiti.

Vurugu za magenge zimeacha zaidi ya Wahaiti 700,000 bila makao huku wengi wakisongamana katika makazi ya muda na yasiyo safi

baada ya nyumba zao kubomolewa. Kulingana na Umoja wa Mataifa zaidi ya watu 5,600 waliripotiwa kuuawa kote Haiti mwaka jana.

Rais William Ruto ambaye amekuwa akipigia debe amani katika taifa hilo la Carribean alisema hivi karibuni kuwa, tangu vikosi vya polisi vya Kenya vitue katika nchi hiyo ambayo imeathiriwa na magenge ya wahalifu, mwanga wa matumiani wa amani umeanza kuonekana hatua ambayo imeanza kurejesha imani ya raia wa Haiti.