Rais wa Kenya awataka vijana kupuuza viongozi wachochezi, asema Uhuru hatawasaidia
-
Rais William Ruto wa Kenya
Rais William Ruto wa Kenya amewataka vijana kuwapuuza viongozi wanaowachochea kuzua fujo na uharibifu wa mali bali wajipange kupata ajira katika miradi na mipango ya serikali yake.
Rais Ruto amewaonya viongozi hao kukoma kuwachochea vijana kushiriki maandamano badala yake amewataka wawaelekeze ili waweze kujiendeleza.
“Vijana wanahitaji mazuri kutoka kwetu kama viongozi. Kwa hivyo, kama viongozi tusiwachochee ili washiriki maandamano ya fujo,” Amesema Dkt William Ruto.
Rais wa Kenya amewahimiza vijana kukataa ushauri wa viongozi kama hao na wajiandae kufaidi kutokana na mipango na miradi ambayo serikali inatekeleza kwa ajili ya kuwapa nafasi za ajira.
Rais Ruto alionekana kumlenga Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye juzi aliwataka vijana wa Gen Z kuendelea kupigania haki zao na utawala bora bila woga.
Majuzi, rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kwa mara ya kwanza alivunja kimya chake kuhusu maandamano ya Gen Z, akiwataka waendelee kutetea haki zao.
Rais huyo wa zamani wa Jamhuri ya Kenya, alisema vijana kwa sasa ndio wenye nguvu na kwamba, hawana budi kupambana na wanaowahujumu. Kenyatta amewahimiza vijana kuendelea na ukakamavu na ujasiri walioonyesha mwaka uliopita, 2024, kufuatia maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali ya Rais William Ruto.
“Mpiganie haki yenu bwana, sio kukaa hapo mali yenu ichukuliwe… Mmeitolea jasho, msikubali… Pambaneni mhakikishe mmepata haki yenu. Mnaskia nyinyi?” alisema Uhuru Kenyatta.