Waislamu Nigeria washerehekea ushindi wa Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121666-waislamu_nigeria_washerehekea_ushindi_wa_wapalestina
Waislamu katika Jimbo la Bauchi, Kaskazini mwa Nigeria, jana Jumapili walisherehekea ushindi wa Wapalestina na Mhimili wa Mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, ambapo kundi la Wazayuni lilisalimu amri mbele ya wanamapambano wa Palestina kwa kukubali mkataba wa kusitisha mapigano.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 20, 2025 04:14 UTC
  • Waislamu Nigeria washerehekea ushindi wa Wapalestina

Waislamu katika Jimbo la Bauchi, Kaskazini mwa Nigeria, jana Jumapili walisherehekea ushindi wa Wapalestina na Mhimili wa Mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, ambapo kundi la Wazayuni lilisalimu amri mbele ya wanamapambano wa Palestina kwa kukubali mkataba wa kusitisha mapigano.

Kiongozi mkuu wa Kiislamu wa kituo cha Bauchi, Sheikh Ahmad Yusuf Yashi ametoa salamu za pongezi kwa taifa la Palestina, harakati ya Hizbullah ya Lebanon, taifa la Yemen, Muqawama wa Iraq na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inaunga mkono na kuongoza mapambano dhidi ya dhulma, uvamizi na ugaidi wa Israel na washirika wake.

“Kwanza, ni muhimu sana kusherehekea ushindi huu kwa sababu unaonyesha uvumilivu na uimara wa Mhimili wa Muqawama, na kupitia makubaliano ya kusitisha mapigano, tunaweza kuona kwa kina na kwa uwazi kabisa kwamba ni ushindi kwa mapambano ya Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni" amesema kiongozi huyo.

Akijibu swali la Iran Press kuhusu kuuawa shahidi viongozi mashuhuri wa Muqawama katika njia ya ukombozi wa al Quds, kiongozi huyo wa kidini amesema: "Kuuawa shahidi watu kama Ismail Haniyah, Yahya Sinwar na wengineo, kamwe hakuwezi kupunguza au kudhuru nguvu ya Muqawama na mapambano ya ukombozi wa Palestina na Quds tukufu." Sheikh Ahmad Yusuf Yashi ameongeza kusema kuwa: "Kuuawa kwao shahidi ni ushindi kwa sababu walipouawa, wanamuqawama wengi waliibuka kuchukua nafasi zao. Kwa hivyo, kamwe sio kushindwa kwa Muqawama, badala yake, ni ushindi wa kambi hiyo."