Polisi Afrika Kusini wamsaka mtuhumiwa wa uchimbaji madini haramu wa Stilfontein
Jeshi la Polisi la Afrika Kusini (SAPS) limeanzisha msako wa kumsaka kiongozi wa uchimbaji madini kinyume cha sheria anayedaiwa kutoroka baada ya kuibuka tena kutoka kwenye mgodi wa dhahabu wa Stilfontein wa Jimbo la Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini-Magharibi wa Afrika Kusini, Patrick Asaneng, jana Jumatatu aliwaagiza maafisa polisi kutumia rasilimali zote wanazoweza kumtafuta mshukiwa ambaye bado hajakamatwa na kuapa kuwatia mbaroni watuhumiwa wote.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Kitaifa wa Jeshi la Polisi SAPS, Athlenda Mathe, mtu anayetafutwa, anajulikana kwa jina la James Neo Tshoaeli maarufu kwa jina la "Tiger," ambaye ni mwenyeji wa Lesotho.
Wachimbaji hao haramu, ambao walikuwa chini ya ardhi tangu mwezi Agosti mwaka jana, walimshutumu Tshoaeli kwa kuiba chakula kilichokusudiwa kwa kila mtu.
Wakati huo huo, mchakato wa kutambua miili 87 ya wachimba migodi haramu, wakiwemo 78 waliopatikana wiki iliyopita, unaendelea. Hayo ni kwa mujibu wa Tshegofatso Mothibedi, Msemaji wa Idara ya Afya Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini.
Mothibedi amewaambia waandishi wa habari kwamba baadhi ya miili hiyo ilikuwa katika hali mbaya ya kuharibika na kuongeza kuwa, baada ya kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba, alama za vidole na kadhalika na kupata uhakika wa wasifu wao, ndipo jamaa wa watu hao wataitwa kuja kukabidhiwa kwa ajili ya hatua za mwisho za maziko.