Raia 16 wa Sudan wauawa katika maandamano Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121716-raia_16_wa_sudan_wauawa_katika_maandamano_sudan_kusini
Polisi nchini Sudan Kusini wamesema kuwa raia 16 wa Sudan waliuawa wakati wa maandamano ya wiki iliyopita nchini humo kama sehemu ya malalamiko yaliyotokea baada ya mauaji ya watu wa Sudan Kusini katika jimbo la Al-Jazira nchini Sudan.
(last modified 2025-01-21T07:32:36+00:00 )
Jan 21, 2025 07:32 UTC
  • Raia 16 wa Sudan wauawa katika maandamano Sudan Kusini

Polisi nchini Sudan Kusini wamesema kuwa raia 16 wa Sudan waliuawa wakati wa maandamano ya wiki iliyopita nchini humo kama sehemu ya malalamiko yaliyotokea baada ya mauaji ya watu wa Sudan Kusini katika jimbo la Al-Jazira nchini Sudan.

Vifo vya watu hao vimethibitishwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi la Sudan Kusini, Kanali John Kassara Koang Nhial, jana Jumatatu.

Wiki iliyopita kulizuka machafuko nchini Sudan Kusini baada ya kuenea video za kutisha kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha raia wa Sudan Kusini waliouawa katika mji wa Wad Madani, makao makuu ya jimbo la Al-Jazira nchini Sudan.

Raia wengi wa Sudan Kusini wanasemekana kukwama katika nchi jirani ya Sudan iliyokumbwa na vita na video hizo ziliamsha moto wa hasira za kulipiza kisasi kwa kuwashambulia raia wa Sudan wanaoishi Sudan Kusini.

Biashara zinazomilikiwa na Wasudan katika vitongoji vyote vya mji wa Juba ziliharibiwa na kuporwa huku mvutano ukizidi kuwa mkubwa.

Serikali ya Sudan ilitoa amri ya kutotoka nje kote nchini humo wiki iliyopita, kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa 12 asubuhi kwa saa za eneo hilo ili kudhibiti uporaji na vurugu.

Polisi wa Sudan Kusini wamesema kwamba, hadi hivi sasa wameshaokoa raia 2,990 wa Sudan ambao kwa sasa wanahifadhiwa na kulindwa kwenye vituo tofauti vya polisi vya mji mkuu Juba.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ametoa mwito kwa utulivu na kukomeshwa kile kinachodaiwa ni ukatili dhidi ya raia wa Sudan Kusini. Amewataka wananchi kuwa watulivu na wajiepushe na kulipiza kisasi.