Waasi wa M23 wauteka mji wa kistratajia mashariki mwa DRC
(last modified Wed, 22 Jan 2025 02:49:11 GMT )
Jan 22, 2025 02:49 UTC
  • Waasi wa M23 wauteka mji wa kistratajia mashariki mwa DRC

Waasi wa M23 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameuteka mji wa mashariki wa Minova, njia kuu ya usambazaji wa bidhaa huko Goma, makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini.

"Minova iko mikononi mwetu," alisema Corneille Nangaa, kiongozi wa Muungano wa Mto Congo unaopinga serikali (AFC), unaojumuisha M23. Mapema mwezi huu wa Januari, waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, waliuteka mji mwingine wa Masisi, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kundi la M23 linaloongozwa na Watutsi limekuwa likiendesha uasi upya katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika ya Kati tangu mwaka 2022. Kongo na Umoja wa Mataifa zinaishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo kupitia msaada wa wanajeshi wake na silaha. Rwanda inakanusha vikali madai hayo.

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufutilia mbali uwezekano wa serikali yake kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na kundi la M23, akisema kwamba hatua hiyo italipa uhalali kundi hilo.

Wanajeshi wa DRC wakishika doria

Kundi la waasi la M23 hivi karibuni lilizidisha mashambulizi yake mashariki mwa DRC na kuteka miji muhimu kama Katale na Masisi na kuwalazimisha watu wengi kukimbia makazi yao.

Kuna makumi ya makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao mashariki mwa Kongo, lakini waasi wa M23 ambao Kinshasa inasema ni wa kabila la Kitutsi linaloungwa mkono na Rwanda, ndilo kundi maarufu zaidi la waasi.