IGAD: Mataifa ya Pembe ya Afrika kushuhudia kiwango kidogo cha mvua
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121758-igad_mataifa_ya_pembe_ya_afrika_kushuhudia_kiwango_kidogo_cha_mvua
Kitengo cha hali ya hewa cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) kimesema kuwa, eneo la Pembe ya Afrika litashuhudia kiwango kidogo cha mvua kuliko kawaida kati ya mwezi Machi na Mei mwaka huu. Ripoti hiyo inatolewa huku Ukanda huo ukiendelea, kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
(last modified 2025-01-22T09:49:18+00:00 )
Jan 22, 2025 09:49 UTC
  • IGAD: Mataifa ya Pembe ya Afrika kushuhudia kiwango kidogo cha mvua

Kitengo cha hali ya hewa cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) kimesema kuwa, eneo la Pembe ya Afrika litashuhudia kiwango kidogo cha mvua kuliko kawaida kati ya mwezi Machi na Mei mwaka huu. Ripoti hiyo inatolewa huku Ukanda huo ukiendelea, kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa mujibu wa ripoti yake ya utabiri wa hali ya hewa, Jumuiya ya IGAD inasema baadhi ya maeneo ya Somalia, Kenya, Ethiopia, Djibouti, Eritrea, Sudan Kusini,  Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania, yatapata mvua za wastani mwezi Machi mwaka huu.

Aidha utabiri unaonesha kuwa maeneo mengi pia yatashuhudia hali ya joto isiyo ya kawaida, hali hii ikitajwa kuwa huenda ikachochea changamoto zaidi za kijamii zinazoshuhudiwa kwenye mataifa hayo.

Abdi Fidar, afisa anayesimamia kitengo cha hali ya hewa cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) IGAD amesema, mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea kushuhudiwa huenda yakaendelea kusababisha ukame, mafuriko na ongezeko la joto, akisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuchukua tahadhari kudhibiti athari zaidi.

Kwa upande wao wataalamu wa masuala ya mazingira, wamewataka wadau kuendelea kuelimisha uma na kuzilinda jamii ambazo ziko katika hatari zaidi.

Mataifa ya Pembe ya Afrika ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi kwani ukame, mafuriko, na wadudu waharibifu huwa jambo la kawaida huku kukiwa na joto la juu la nyuzi joto 32, kulingana na kituo hicho.