Kenya yarahisisha masharti ya safari kwa karibu nchi zote Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121760-kenya_yarahisisha_masharti_ya_safari_kwa_karibu_nchi_zote_afrika
Kenya imetangaza kuwa, itawaruhusu raia wa karibu mataifa yote ya Afrika kuzuru nchini humo bila kuhitaji idhini ya awali. Hiyo ni kulingana na agizo jipya la baraza la mawaziri la nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
(last modified 2025-01-22T09:49:45+00:00 )
Jan 22, 2025 09:49 UTC
  • Kenya yarahisisha masharti ya safari kwa karibu nchi zote Afrika

Kenya imetangaza kuwa, itawaruhusu raia wa karibu mataifa yote ya Afrika kuzuru nchini humo bila kuhitaji idhini ya awali. Hiyo ni kulingana na agizo jipya la baraza la mawaziri la nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Mwaka jana, Kenya ilianzisha sera ya "bila visa" ambayo ilihitaji wageni wengi kutuma maombi mtandaoni ili kupata idhini kabla ya kuondoka nchini mwao.

Lakini kuanzishwa kwa Idhini ya Usafiri wa Kielektroniki (ETA), ambayo ilichukua nafasi ya hitaji la visa kwa wageni wote, ilikosolewa kama "visa chini ya jina lingine".

Siku ya Jumanne, taarifa ya baraza la mawaziri ilisema ETA itaondolewa kwa "nchi zote za Afrika isipokuwa Somalia na Libya - kutokana na sababu za kiusalama".

Taarifa ya serikali ya Kenya ilisema, hii ni sehemu ya "juhudi za kuunga mkono sera za wazi na ukuaji wa utalii" na "kukuza ushirikiano wa kikanda sambamba na na kurahisisha usafiri katika bara zima".

Hata hivyo, licha ya kuanzisha ETA, Kenya ilifanya vibaya zaidi katika orodha ya hivi punde ya jinsi ilivyo wazi kwa wageni, ikishuka nafasi 17 hadi 46 kati ya mataifa 54 katika Orodha ya Uwazi ya Visa ya Afrika ya 2024.

Nchi kadhaa za Afrika zimejaribu kurahisisha mahitaji ya usafiri kwa wageni kutoka kwingineko barani humo katika miaka ya hivi karibuni hatua ambayo inalenga kuboresha sekta ya utalii.