Balozi wa Palestina Ghana: Ari ya mapambano ya Wapalestina kamwe haitazimwa
Balozi wa Palestina nchini Ghana amesema kuwa, ari na moyo wa mapambano ya Wapalestina kamwe haitazimwa na kwamba, Wapalestina wataendelea kusimama kidete kupigania haki zao.
Balozi wa Palestina nchini Ghana, Abdul Fatah Alsattari, amekaribisha kwa mikono miwili usitishaji vita wa Gaza, akibainisha umuhimu wa uthabiti wa Wapalestina na hitaji lao la haraka la amani na uhuru.
Balozi wa Palestina nchini Ghana amesema, ni muhimu kwa kuangazia mzozo wa kina wa kibinadamu unaowakabili Wapalestina, akikumbusha kwsamba, mizozo hii ina athari kubwa za kibinadamu na inahitaji umakini wa kimataifa kwa haki na amani.
Mwakilishi huyo wa Palestina nchini Ghana ameeleza wazi kwamba, licha ya mateso makubwa, wananchi wa Palestina kamwe hawatasalimu amri na wamejitolea kutafuta uhuru na amani. Vile vile amezungumzia jinai za kivita zinazofanywa na Israel na athari zake katika maisha ya kila siku kwa Wapalestina, akiitaka jumuiya ya kimataifa kuzingatia hali hiyo.
Amewashukuru wale wote waliounga mkono kadhia ya Palestina na kusisitiza umuhimu wa mshikamano wa kimataifa dhidi ya dhulma na ukandamizaji.
Aidha balozi Abdul Fatah Alsattari ameelaani jinai za Israel, akisisitiza kwamba, mzozo kati ya Israel na Wapalestina umekita mizizi katika historia na utambulisho wa Wapalestina, ambao mapambano yao yanayoendelea ya amani na uhuru yanahitajia kuungwa mkono na kimataifa.