Maelfu wakimbia makazi yao DRC baada ya waasi wa M23 kuingia Sake
Hali ya wasiwasi imetanda katika mji wa Goma, ambapo maelfu ya watu wanakimbia kutokana na mapigano makali kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kundi la waasi wa M23.
Wakati waasi hao wanaodaiwa kuungwa mkono na jeshi la Rwanda, wakiteka mji wa SAKE, wakazi wengi wanajikuta wakiwa na hofu na kukosa mahali pa kwenda.
Wakazi wameketi kando ya barabara wakiwa na mifugo na mizigo yao, bila kujua hatima yao. Hali hii inatokana na kuongezeka kwa ghasia na mapigano, ambapo waasi wa M23 wamefanikiwa kuteka mji wa Sake, ulioko yapata umbali wa kilomita 20 kutoka Goma.
Raia wanaokimbia kutoka katika baadhi ya makambi karibu na mji wa Goma wakihofia usalama wao wanasema. Tayari waasi hao wameudhibiti mji muhimu wa Minova ulioko Kongo Mashariki.
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo hata hivyo linashambulia kwa mizinga maeneo yote yanayozungukwa na mji huo wa Sake ambamo raia wote wamekimbia. Huku waasi wakisonga mbele wakipiga roketi kuelekea sasa kijiji cha Mubambiro karibu na kambi za wakimbizi mjini Goma. Aline KAHINDO ni mmoja wa wakimbizi hao ambaye bado anahangika kupata sehemu ya kukimbilia.
Hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imezorota kwa kiasi kikubwa. Hivi sasa kunashuhudiwa kuongezeka migogoro inayohusisha makundi mbalimbali yenye silaha, hususan waasi wa M23 na ADF.
Mgogoro unaoendelea mashariki mwa DRC umezidisha hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo na kusababisha zaidi ya watu milioni 7 kuyahama makazi yao.