Dozi milioni 10 za chanjo ya Malaria zapatiwa bara la Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121834-dozi_milioni_10_za_chanjo_ya_malaria_zapatiwa_bara_la_afrika
Shirika la Kimataifa linaloshughulika na kuboresha upatikanaji wa chanjo la Gavi limetangaza kuwa, karibu dozi milioni 10 za Malaria zilipelekwa Afrika katika mwaka wa kwanza wa utoaji chanjo kote barani humo.
(last modified 2025-01-24T03:28:29+00:00 )
Jan 24, 2025 03:28 UTC
  • Dozi milioni 10 za chanjo ya Malaria zapatiwa bara la Afrika

Shirika la Kimataifa linaloshughulika na kuboresha upatikanaji wa chanjo la Gavi limetangaza kuwa, karibu dozi milioni 10 za Malaria zilipelekwa Afrika katika mwaka wa kwanza wa utoaji chanjo kote barani humo.

Hatua hiyo ni katika juhudi za kuudhibiti ugonjwa wa Malaria ambao kulingana na Shirika la Afya Duniani  (WHO) unauwa karibu watu 600,000 kwa mwaka duniani kote wengi wao wakiwa ni watoto.

Katika awamu ya kwanza ya majaribio ya utoaji wa chanjo kwa mwaka 2019 hadi 2023, zaidi ya watoto milioni mbili walipatiwa chanjo ya Malaria aina ya RTS, S kwenye mataifa ya Ghana, Kenya na Malawi. Matokeo yake kulishuhudiwa kupungua kwa wagonjwa wa Malaria na watu wanaolazwa hospitali kutokana na maradhi hayo.

Kulingana na Shirika la Afya duniani WHO, idadi ya vifo imepungua kwa asilimia 13 na sasa linapendekeza chanjo ya RTS s itumike sambamba na chanjo aina ya R21/Matrix-M katika kupambana na Malaria.

Baada ya awamu ya kwanza kutolewa, chanjo hiyo ilipelekwa kwenye nchi hizo tatu na nyingine 14 ambako ilianzia Cameroon Januari 2014. Shirika la kimataifa la kuboresha upatikanaji wa chanjo la Gavi limesema tangu wakati huo, dozi nyingine milioni 9.8 zimeshatolewa na kukadiria kuwa takriban watoto milioni tano wamepata kinga kwa kiasi fulani.

Shirika hilo limesema mpango wa utoaji chanjo za Malaria unakusudia kutoa dozi nne za chanjo hizo kwa kila mtoto. Gavi, limepongeza matokeo ya awali ya chanjo hizo nchini Cameroon kwa kufanikiwa kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.