Yahya Jammeh Rais wa zamani wa Gambia kurejea kutoka uhamishoni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121840-yahya_jammeh_rais_wa_zamani_wa_gambia_kurejea_kutoka_uhamishoni
Yahya Jammeh Rais wa zamani wa Gambia ametangaza kuwa, ana nia ya kuchukua tena udhibiti wa chama chake cha siasa na kutangaza kwamba “anarudi nyumbani”.
(last modified 2025-01-24T05:47:22+00:00 )
Jan 24, 2025 05:47 UTC
  • Yahya Jammeh Rais wa zamani wa Gambia kurejea kutoka uhamishoni

Yahya Jammeh Rais wa zamani wa Gambia ametangaza kuwa, ana nia ya kuchukua tena udhibiti wa chama chake cha siasa na kutangaza kwamba “anarudi nyumbani”.

Jammeh amesema hayo katika ujumbe wa sauti ambao duru za habari zimeupata.

Jammeh alitawala taifa hilo dogo la Afrika Magharibi kwa miaka 22, akiongoza serikali iliyotuhumiwa kutekeleza mateso, kutumia magenge yanayoua watu na kufanya dhulma nyingine nyingi.

Jammeh amekua akiishi uhamishoni nchini Equatorial Guinea tangu mwaka 2017 baada ya kushindwa katika uchaguzi na rais wa sasa Adama Barrow, lakini bado ana wafuasi wengi nchini mwake na ameonyesha mara nyingi nia ya kurejea kwenye ulingo wa siasa.

“Leo, nimeamua kuchukua chama changu mwenyewe na sitakikabidhi kwa mtu yeyote,” Jammeh alisema katika ujumbe wa sauti uliotumwa kwa wafuasi wake kutoka chama cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction (APRC) .

“Kama kuna mtu yeyote anapenda au asipende, kwa uwezo na neema ya Mwenyezi Mungu, nitarudi.”

Jammeh ametoa tangazo hilo mwezi mmoja baada ya Jumuia ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS kuiunga mkono mahakama maalum ya mseto kutoa hukumu kwa uhalifu uliotendwa wakati wa utawala wake.

Mwaka 2022 serikali ya Gambia iliidhinisha mapendekezo ya tume iliyochunguza ukatili uliofanywa wakati wa utawala wa Yahya Jammeh, huku maafisa wakikubali kuwashtaki watu 70 akiwemo rais huyo wa zamani, aliyeingia madarakani kufuatia mapinduzi ya mwaka 1994.