Watu zaidi ya 200 wauawa na waasi wa M23 Kivu Kusini DRC
Zaidi ya raia 200 wanariipotiwa kuuawa na waasi wa M23 katika baadhi ya vijiji vya kundi la Buzi na sehemu ya Mbinga Nord huko Kalehe, katika jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hiyo ni kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari vya eneo hilo ambavyo vimeripoti pia juu ya kuweko mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa kundi hilo la waasi.
Baadhi ya ripoti zinafichua kuwa, maeneo hayo yanashuhudia ukiukaji mkuubwa wa haki za binadamu huku wasiwasi ukitanda kutokana na kuzidi kuzorota usalama katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wakati huo huo, hali ya wasiwasi imetanda katika mji wa Goma, ambapo maelfu ya watu wanakimbia kutokana na mapigano makali kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kundi la waasi wa M23.
Wakati waasi hao wanaodaiwa kuungwa mkono na jeshi la Rwanda, wakiteka mji wa SAKE, wakazi wengi wanajikuta wakiwa na hofu na kukosa mahali pa kwenda.
Hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imezorota kwa kiasi kikubwa. Hivi sasa kunashuhudiwa kuongezeka migogoro inayohusisha makundi mbalimbali yenye silaha, hususan waasi wa M23 na ADF.
Mgogoro unaoendelea mashariki mwa DRC umezidisha hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo na kusababisha zaidi ya watu milioni 7 kuyahama makazi yao.