Sheikh Zakzaky awaenzi watoto wa Mashahidi wa Nigeria, Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121886-sheikh_zakzaky_awaenzi_watoto_wa_mashahidi_wa_nigeria_palestina
Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria aliandaa dhifa ya chakula cha jioni Ijumaa usiku kwa ajili ya kuzienzi familia za wafuasi wake waliopoteza maisha katika harakati za kupigania haki nchini Nigeria na katika kadhia ya Palestina.
(last modified 2025-01-25T11:33:49+00:00 )
Jan 25, 2025 11:33 UTC
  • Sheikh Zakzaky awaenzi watoto wa Mashahidi wa Nigeria, Palestina

Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria aliandaa dhifa ya chakula cha jioni Ijumaa usiku kwa ajili ya kuzienzi familia za wafuasi wake waliopoteza maisha katika harakati za kupigania haki nchini Nigeria na katika kadhia ya Palestina.

Iran Press imeandika habari hiyo na kueleza kuwa, shara hiyo ililenga kuhakikisha kwamba, kuuawa shahidi wazazi na wapendwa wao hakiwasababishi changamoto kubwa za kijamii, kihisia, na nyinginezo, na pia kuhakikisha kwamba watoto wanabaki kwenye njia ya Muqawama ambayo wazazi wao walisabilia maisha yao ya thamani kwayo.

Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria chini ya uongozi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky kwa zaidi ya miaka 30 imekuwa ikizienzi familia za wanachama wake waliouawa shahidi. Marasimu hayo yalifanywa katika mkesha wa Siku ya Mashahidi inayoadhimishwa kila mwaka, maarufu kwa jina la Yaumu Shuhada kila tarehe 25 Rajab, tarehe ambayo Imam Musa Al Kadhim AS, Imam wa saba wa Shi'a aliuawa shahidi.

Katika mhadhara wake kwa watoto hao mjini Abuja, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria alisema "Lazima muendeleze yale ambayo wazazi wenu walikuwa wakiyafanya wakati wa uhai wao, yaani kupinga dhulma. Wametekeleza ahadi zao kwa Mwenyezi Mungu, na tunaamini kuwa kwa sasa wapo Mbinguni pamoja na watumishi wema."

Sheikh Ibrahim Zakzaky

Hali kadhali Sheikh Zakzaky amewataka watoto hao kuendelea kuwakumbuka na kuwaombea wazazi wao daima.

Kuna maelfu ya watoto na familia za mashahidi nchini Nigeria, wengi wao walipoteza wazazi na walezi wao wakati wa mauaji ya Zaria 2015, wakati wanajeshi wa Nigeria chini ya amri ya Rais wa wakati huo Muhammadu Buhari walipovamia Hussainiyyah ya Baqiyyatullah katika mji wa Zaria, misikiti, na makazi ya Sheikh Zakzaky, na kuua zaidi ya 1000 ya Waislamu wa Kishia 1000 wasio na silaha na uloinzi, wakiwemo wanawake na watoto.