Mapigano Sudan yaharibu kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta
Mapigano yanayoendelea karibu na kiwanda kikubwa zaidi cha kusafisha mafuta nchini Sudan yamesababisha moto mkubwa.
Jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF wametupiana lawama kwa kusababisha moto huo.
Kiwanda hicho cha al-Jaili kinachopatikana umbali wa takriban kilometa 60 kaskazini mwa mji mkuu Khartoum ni mali ya serikali ya Sudan na kampuni ya mafuta inayomilikiwa pia na serikali ya China, na kina uwezo wa kusafisha mapipa 100,000 ya mafuta kwa siku.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea wasiwasi wake kufuatia mapigano makali huko Sudan huku akizitaka pande zote kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kuwa na matokeo hatari kwa Sudan na ukanda mzima, ikiwa ni pamoja na athari kubwa za kiuchumi na kimazingira.
Kinu hicho ni kinu kikubwa zaidi cha kusafisha mafuta huko Sudan; na kimekuwa kikidhibitiwa na wanamgambo hasimu wa RSF tangu kuibuka mzozo huko Sudan mwezi Aprili mwaka 2023. Hayo yanajiri katika hali ambayo, Mkuu wa Baraza la Utawala na Kamanda wa Jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, amesisitiza kuwa, makundi yanayoliunga mkono jeshi hayatanyakua madaraka baada ya vita vya ndani nchini humo.
Al Burhan ameahidi kutoruhusu ushindi wa watu wa Sudan kutekwa nyara na kundi moja la watu, na kwamba makundi yanayoliunga mkono jeshi hayatahodhi madaraka ya nchi baada ya vita, akisisitiza kuwa vikosi vya kijeshi vinasimama katika safu moja na makundi mengine.