Maiti zazagaa barabarani, hospitali zaelemewa na majeruhi huku mapigano yakishtadi Goma, DRC
Mapigano makali yanaendele kati ya wapiganaji wa M23 na wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC katika mji wa Goma mashariki mwa nchi hiyo huku yakiacha maiti nyingi zikiwa zimezagaa mitaani, na hospitali nazo zikielemewa na ongezeko la majeruhi.
Siku ya Jumatatu, waasi wa M23 ambao Umoja wa Mataifa unasema wanaungwa mkono na Rwanda, waliingia mjini Goma na kutangaza kuwa wameuteka na kuudhibiti mji huo muhimu kuashiria pigo kubwa kwa jeshi la Kongo na kuongezeka kwa mzozo wa miaka mingi ambao umesababisha vifo vya mamia ya watu na kuwahamisha mamilioni ya wengine katika eneo hilo.
Hata hivyo Waziri wa Maendeleo ya Vijijini wa DRC Muhindo Nzangi alisema jeshi la serikali lingali linadhibiti asilimia 80 ya eneo la mji wa Goma, ambao ni makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini.
Katika kikao na wanahabari siku ya Jumanne, Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yalitahadharisha kuwa hospitali katika mji wa Goma zimeelemewa kwa kuzidiwa na majeruhi, zikiwatibu mamia ya wagonjwa waliojeruhiwa kwa risasi na makombora huku miili mingi ya watu waliouawa ikiwa imezagaa mitaani.
Wakati huo huo, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limesema, shughuli za usambazaji misaada ya chakula ndani na karibu na Goma "zimesitishwa kwa muda" na kuelezea wasiwasi lilionao wa kuwepo uhaba wa chakula.
Mapigano makali yanayoripotiwa kuendelea katika mji wa Goma yamepelekea maelfu ya watu kumiminika nje ya mji huo, ambao umekuwa kitovu kikuu cha utoaji misaada ya kibinadamu kwa watu waliolazimika kuyahama makazi yao. Mamia kwa maelfu ya watu wamekimbia mapigano tangu ulipoanza mwaka huu mbali na wengine milioni tatu waliohama makazi yao mwaka jana huko mashariki mwa DRC.../