UN: Watu 700 wameuawa DRC ndani ya siku tano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122178-un_watu_700_wameuawa_drc_ndani_ya_siku_tano
Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kukomesha ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 yamesababisha watu zaidi ya 700 kuuawa huku wengine wasiopungua 2,800 wakijeruhiwa katika kipindi cha siku tano.
(last modified 2025-02-01T04:29:31+00:00 )
Feb 01, 2025 04:29 UTC
  • UN: Watu 700 wameuawa DRC ndani ya siku tano

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kukomesha ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 yamesababisha watu zaidi ya 700 kuuawa huku wengine wasiopungua 2,800 wakijeruhiwa katika kipindi cha siku tano.

Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja na washirika wa serikali, wamefanya tathmini ambayo ilifichua hali ya kuogofya ya mgogoro huo wa eneo la mashariki mwa DRC. Maafisa wameonya kwamba, idadi hiyo huenda ikaongezeka kadiri habari zaidi zinavyopatikana.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametoa wito wa kukomeshwa ghasia zinazoongezeka katika eneo hilo, na kuonya kuhusu hali mbaya zaidi katika mji wa Goma, ambao ni makazi ya takriban watu milioni 3.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetoa tahadhari kuhusu kupungua kwa usambazaji wa chakula, maji safi na suhula za matibabu.

"Watu wanakosa chakula, maji safi, vifaa vya matibabu, na kwa msingi huo tuna wasiwasi mkubwa," msemaji wa WFP, Shelley Thakral amesema na kuongez kuwa, "Mgogoro huo unachangiwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu."

Wapiganaji wa M23

Angalau kambi mbili za wakimbizi wa ndani (IDP) zilishambuliwa kwa mabomu, kuwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR). Shirika hilo la haki la UN pia limeleza habari ya kuuawa kinyume cha sheria watu wasiopungua 12 na waasi wa M23 kati ya Januari 26 na 28.

Waasi wa kundi la M23 la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linaloungwa mkono na Rwanda, ambalo limeteka mji mkubwa zaidi mashariki mwa nchi hiyo, Goma, wametangaza nia yao ya kupeleka vita katika mji mkuu, Kinshasa, huku Rais Félix Tshisekedi akitoa wito wa kuandaliwa jeshi kubwa kukabiliana na mashambulizi hayo.