Rais Rouhani amlaki rasmi Rais Dramani Mahama wa Ghana
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemlaki na kumkaribisha rasmi Rais John Dramani Mahama wa Ghana katika jengo la kiutamaduni na kihistoria la Ikulu ya Sa'ad Abad mjini Tehran.
Katika hafla hiyo iliyofanyika leo asubuhi, baada ya kupigwa nyimbo za taifa za nchi mbili, Marais wa Iran na Ghana walikagua gwaride la heshima na kutambulishana jumbe za ngazi za juu za maafisa wa nchi mbili.
Imeelezwa kuwa mazungumzo ya marais wa Iran na Ghana katika vikao vitakavyojumuisha jumbe za ngazi za juu za nchi mbili na kusainiwa hati kadhaa za ushirikiano wa pande mbili ni miongoni mwa ratiba za Rais wa Ghana katika safari yake hapa nchini.
Kustawisha na kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili kieneo na kimataifa na vilevile kuinuia kiwango cha ushirikiano katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kibiashara na kiutamaduni baina ya Tehran na Accra ni miongoni mwa malengo ya safari rasmi ya Rais John Dramani Mahama wa Ghana hapa nchini.
Rais wa Ghana, akiandamana na ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yake aliwasili mjini Tehran jana usiku na kulakiwa na Waziri wa Jihadi ya Kilimo ambaye ndiye mwenyekiiti wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano ya Iran na Ghana.../