Utulivu wa kulegalega washuhudiwa Goma; Mapigano yapungua mashariki mwa DRC
Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa licha ya kurejea utulivu wa kiwango fulani katika mji wa Goma, makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mashirika ya misaada ya kibinadamu yameonya juu ya kushtadi hali ya mambo huku hospitali zikizidiwa na wagonjwa, uhaba wa vifaa muhimu vya tiba ukishuhudiwa na miili ya watu waliouawa ikiendelea kuonekana mitaani.
Mapigano yaliibuka katika mji wa Goma wiki iliyopita wakati waasi wa kundi la M23 walipoanzisha mshambulizi dhidi ya vikosi vya serikali ya Kinshasa. Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 700 na kujeruhi 2,800 katika muda wa siku tano zilizopita.
Maelfu ya wananchi wa Kongo wamekuwa wakimbizi, wengi wakikimbilia katika nchi jirani ya Rwanda, wakiwemo wafanyakazi wa taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia.
Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imesema kuwa mji wa Goma unaendelea kutatizwa na changamno kubwa licha ya hali ya maisha kurejea polepole katika hali ya kawaida huku huduma ya usafiri na masoko ikiendelea kufungwa.
Wakati huo huo Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na washirika wengine wa serikali zimefanya tathmiani iliyofichua madhara makubwa ya mgogoro wa mashariki mwa Kongo.
Nao Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umetahadharisha kuhusu kupungua kwa usambazaji chakula, maji safi na vifaa tiba.