Afrika Kusini yamuonya Trump; Tutasitisha mauzo ya madini kwa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122324-afrika_kusini_yamuonya_trump_tutasitisha_mauzo_ya_madini_kwa_marekani
Waziri wa Madini na Rasilimali za Petroli wa Afrika Kusini, Gwede Mantashe ametoa wito kwa nchi za Afrika kusimamisha mauzo ya madini kwenda Marekani.
(last modified 2025-02-05T02:41:26+00:00 )
Feb 05, 2025 02:41 UTC
  • Afrika Kusini yamuonya Trump; Tutasitisha mauzo ya madini kwa Marekani

Waziri wa Madini na Rasilimali za Petroli wa Afrika Kusini, Gwede Mantashe ametoa wito kwa nchi za Afrika kusimamisha mauzo ya madini kwenda Marekani.

Mwito huo umekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza mipango ya kuikatia misaada Afrika Kusini kutokana na eti sera zake za unyakuzi wa ardhi. Siku ya Jumapili, Trump bila kutoa ushahidi wowote alidai kuwa "matabaka fulani ya watu" nchini Afrika Kusini yanabaguliwa na kunyanyaswa.

Akizungumza katika Kongamano la Uwekezaji wa Madini ya Afrika la Indaba mjini Cape Town, Mantashe amesema kuwa, mataifa ya Afrika hayapaswi kuogopa vitisho vya Marekani. "Tuzuie madini kwenda Marekani," waziri huyo amesema.

Ameeleza bayana kuwa, "Kama hawatupi pesa, tusiwape madini ... sisi sio ombaomba, tuitumie jaala hiyo (madini) kwa manufaa yetu. Kama bara iwapo tutadumaa kwa hofu, tutaanguka, lakini na madini mlangoni kwetu.”

Rais wa Marekani, Donald Trump

Hii ni katika hali ambayo, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini juzi Jumatatu alipinga bwabwaja hizo za Trump na kusema kuwa, Pretoria haijawahi kunyakua ardhi yoyote ile. Ramaphosa alisema, kampeni inayofanyika Afrika Kusini ni mchakato wa kisheria ulioidhinishwa kikatiba ambao unataka kuhakikisha kwamba raia wote wanapata ardhi kwa njia sahihi, kiuadilifu na kwa haki kama inavyoelekezwa na katiba. 

Pia alifichua kuwa: "Hakuna ufadhili mwingine zaidi ya wa VVU unaopokelewa na Afrika Kusini kutoka Marekani," ikiwa ni kuashiria kwamba amemtaka Trump asiidangaye dunia kwamba Marekani inatoa msaada mkubwa kwa Afrika Kusini na hivyo ina haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.