Maafisa wa SADC na EAC watilia mkazo kusitishwa mapigano mashariki mwa Kongo
Maafisa wa ngazi ya juu kutoka mataifa ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika jana walitilia mkazo kusitishwa mara moja mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuzitaka pande zote husika kutoa kipaumbele kwa suala la kufanya mazungumzo ili kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.
Musalia Mudavadi Waziri Kiongozi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya ambaye alisimamia mkutano huo wa jana ametilia mkazo udharura wa kuhitimisha uhasama na kutoa kipaumbele kwa suala la kufanya mazungumzo ili kutatua mgogoro wa mashariki mwa Kongo.
"Amani sio kama kahawa ya papo hapo. Huwezi kuitengeneza. Tuna wakati mzuri kama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuwasaidia watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo," amesema Mudavadi mbele ya wajumbe katika mkutano uliofanyika katika ngazi ya mawaziri nchini Tanzania jana Ijumaa.
Amon Murwira Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe mwenyekiti mwenza mwingine, aliunga mkono maoni ya Mudavadi, na kuongeza kuwa majadiliano yao yameanda mazingira ya mkutano wa wakuu wa nchi na serikali uliopangwa kufanyika leo Jumamosi, ambapo Marais wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo watakutana nchini Tanzania kutafuta suluhu ya kadhia ya mashariki mwa Kongo.
Hii ni katika hali ambayo kutohudhuria Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mkutano wa karibuni wa EAC uliofanyika kwa njia ya mtandao kuliibua wasiwasi kuhusu kujitolea kwake katika mazungumzo ya kikanda.
Akizungumza jana katika kikao maalumu cha Baraza la Haki za Binadamu la UN mjini Geneva Uswisi, Volker Turk Kamisha Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alilaani kuendelea machafuko mashariki mwa Kongo na kusema tangu Januari 26 mwaka huu hadi sasa karibu watu 3,000 wameuawa na 2,880 kujeruhiwa. Aidha watu zaidi ya laki tano wamelazimika kuhama makazio yao kutokana na mapigano yanayoendelea mashariki mwa Kongo.