Waafrika Kusini 'weupe' wakataa 'ofa' ya kuwa wakimbizi Marekani
Raia wa Afrika Kusini wenye asili ya Uholanzi na nchi nyingine za Ulaya wamepuuzilia mbali mwito wa Rais Donald Trump, wa kwenda kuwa wakimbizi nchini Marekani, kwa madai ya kubaguliwa nchini Afrika Kusini.
Kallie Kriel, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Afriforum linalopigania maslahi ya jamii ya Waafrikana amemhutubu Trump kwa kumwambia, “Hatutaki kuhamia kwingine, na hatutawaomba watoto wetu wahamie nchi nyingine. Tuna maslahi ya vizazi vijavyo na kuhakikisha utamaduni wetu unapitishwa kwa vizazi vijavyo; hilo haliwezi kufanyika nje ya nchi.”
Kiongozi wa kikundi hicho cha wazungumzaji wa Kiafrikana amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu, Pretoria na kuongeza kuwa, mustakabali wa Waafrikana, ambao ni wazawa wa walowezi wa Ulaya, upo barani Afrika.
"Sisi si Wazungu. Sisi ni wazawa wa nchi hii na hatuendi popote," ameuambia mkutano wa pamoja wa vyombo vya habari na chama cha wafanyakazi cha Solidarity Movement.
Msimamo huo wa Waafrikana (Afrikaners) unakuja baada ya Trump kupasisha amri ya utendaji siku ya Ijumaa ya kukata misaada wa Washington kwa Pretoria, kutokana na kile alichodai kuwa sheria ya ugawaji wa ardhi iliyopitishwa hivi karibuni, na kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel iliyowasilishwa na Afrika Kusini katika mahakama za kimataifa.
Ikijibu madai ya Trump kuwa eti Marekani haiwezi kuunga mkono sera ya marekebisho ya ardhi ya Afrika Kusini Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imesema kuwa, hatua hiyo ya Washington ni ukiukaji wa haki ya kujitawala Afrika Kusini, na kwamba inasikitisha kuona kwamba propaganda hizo zinafanywa na wakuu wa kutoa maamuzi nchini Marekani.