Maandamano ya kumuunga mkono Rais Kabila wa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12265-maandamano_ya_kumuunga_mkono_rais_kabila_wa_drc
Maelfu ya wafuasi wa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walijitokeza mabarabarani hapo jana Ijumaa na kufanya maandamano ya kumuunga mkono kiongozi huyo, siku mbili baada ya wafuasi wa Etienne Tshishekedi, kiongozi mkongwe wa upinzani kurejea nchini baada ya kuwa nje ya nchi kwa zaidi ya miaka miwili na kukaribishwa kwa maandamano makubwa ya kumuunga mkono.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 30, 2016 03:37 UTC
  • Maandamano ya kumuunga mkono Rais Kabila wa DRC

Maelfu ya wafuasi wa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walijitokeza mabarabarani hapo jana Ijumaa na kufanya maandamano ya kumuunga mkono kiongozi huyo, siku mbili baada ya wafuasi wa Etienne Tshishekedi, kiongozi mkongwe wa upinzani kurejea nchini baada ya kuwa nje ya nchi kwa zaidi ya miaka miwili na kukaribishwa kwa maandamano makubwa ya kumuunga mkono.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, zaidi ya wafuasi 40,000 wa Rais Kabila walishiriki maandamano hayo yaliyofanyika katika mji mkuu Kinshasa ambapo baadhi yao walisikika wakipiga nara kama, "Kabila bakia madarakani kwa muda utakao". Aidha waandamanaji hao walikuwa wamevalia fulana zenye picha za Kabila huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kumuunga mkono rais huyo.

Maandamano ya kumuunga mkono Etienne Tshisekedi, kinara wa upinzani DRC

Jumatano iliyopita, maelfu ya wafuasi wa Mzee Etienne Tshisekedi walifurika katika uwanja wa ndege na vilevile kujipanga katika barabara ya kuelekea kwao Limete kumlaki kiongozi huyo mkongwe wa upinzani ambaye kurejea kwake nchini kunatarajiwa kupiga jeki harakati za wapinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa rais. Mwanasiasa huyo anatarajiwa kujiunga na viongozi wengine wa upinzani hapo kesho kwa ajili ya maandamano na mkutano wa kisiasa wenye lengo la kimshinikiza Rais Joseph Kabila kutoakhirisha uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini humo mwishoni mwa mwaka huu.

Rais Joseph Kabila wa DRC anayetuhumiwa na wapinzani kun'gang'ania madaraka

Rais Kabila anayemaliza muhula wake wa uongozi mwaka huu, amekuwa akitoa wito mara kwa mara wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa, wito ambao umekuwa ukipingwa na wapinzani wanaosema ni njama ya serikali kutaka kuakhirisha uchaguzi wa rais wa Novemba mwaka huu na hivyo kuongeza muda wa Kabila kuendelea kuweko madarakani.