Bunge la Tunisia lapiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12322-bunge_la_tunisia_lapiga_kura_ya_kutokuwa_na_imani_na_waziri_mkuu
Bunge la Tunisia limepitisha kwa wingi mkubwa, kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Habib Essid.
(last modified 2026-01-05T06:17:05+00:00 )
Jul 31, 2016 07:42 UTC
  • Bunge la Tunisia lapiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu

Bunge la Tunisia limepitisha kwa wingi mkubwa, kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Habib Essid.

Serikali ya Essid imekuwa chini ya mashinikizo kwa muda wa miezi miwili sasa tangu Rais Beji Caid Essebsi wa nchi hiyo alipotangaza kuwa anaunga mkono kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Kati ya wabunge wote 217 wa bunge la Tunisia, wabunge 191 walishiriki katika upigaji kura ambapo 118 waliunga mkono hoja ya kutokuwa na imani na serikali ya Waziri Mkuu Habib Essid ambaye ameshikilia wadhifa huo kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Ni wabunge watatu tu walimuunga mkono Essid na waliosalia waliamua kutopiga kura. 

Bunge la Tunisia

Akihutubia bunge kabla ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye, Essid mwenye umri wa miaka 67 alisisitiza kuwa aliukubali wadhifa wa Uwaziri Mkuu kwa sababu ya kutekeleza jukumu la kitaifa tu wala hana nia ya kung'ang'ania kushika cheo hicho. Alisema hakwenda bungeni kwa lengo la kupata kura 109 za kumwezesha kuendelea kushika wadhifa wa Uwaziri Mkuu.

Waziri Mkuu wa Tunisia aliyeuzuliwa ameongeza kuwa:"Ninajua kwamba bunge halitoipigia serikali kura ya kuwa na imani nayo lakini nimefadhilisha kuheshimu Katiba na nitaridhia uamuzi wowote utakaopitishwa na bunge".

Waziri Mkuu wa Tunisia Habib Essid kabla ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye bungeni

Habib Essid amekuwa akikosolewa na vyama vyote kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kushindwa kutatua matatizo ya kiuchumi na kisiasa yanayoikabili nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.../