Jul 31, 2016 13:47 UTC
  • Maandamano ya raia wa Mali ya kuunga mkono maridhiano ya kitaifa

Maelfu ya wananchi wa Mali wameshiriki katika maandamano makubwa ya kuunga mkono makubaliano ya amani na makundi ya wabeba silaha nchini.

Barabara za Bamako, mji mkuu wa Mali Jumamosi ya jana, zilishuhudia maandamano ya maelfu ya raia walioandamana kuunga mkono maridhiano ya kitaifa. Waandamanaji walitaka kutekelezwa haraka vipengee vya makubaliano hayo ya amani na serikali ili kuhitimishwa machafuko na ghasia hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. Kikao cha wanamgambo nchini Mali chini ya fremu ya utekelezwaji wa makubaliano ya amani na serikali ya Bamako, kilifanyika kitambo kidogo nyuma kwa usimamizi wa Brigi Rafini, Waziri Mkuu wa Niger ambapo makundi hayo ya wabeba silaha yalikubali kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kudhamini usalama wa mji wa Kidal, kaskazini mwa nchi sanjari na kupunguza migogoro ndani ya nchi hiyo. Mwishoni mwa kikao hicho kilichofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 14-17 mwezi huu wa Julai huko mjini Niamey, Niger wanamgambo wanaoendesha harakati zao eneo la Kidal, kaskazini mwa Mali likiwemo kundi la waasi liitwalo Uratibu wa Harakati za Azawad (CMA) na wanamgambo wanaounga mkono serikali ya Rais Ibrahim Boubacar Keïta wa nchi hiyo, kwa pamoja walitoa ripoti ambayo kwa mujibu wake walikubaliana kupunguza migogoro sanjari na kusisitizia juu ya kudhibiti hali ya mambo kwa namna iliyo bora.

Mali maandamano ya wananchi

Washiriki katika maandamano ya jana pia walitangaza uungaji wao mkono kwa jeshi la serikali ya Mali, huku wakilaani vikali hujuma ya hivi karibuni ya wanamgambo dhidi ya askari na kusababisha 17 kati yao kuuawa. Inafaa kuashiria kuwa, siku chache tu baada ya kutiwa saini makubaliano hayo ya amani, kuliibuka mapigano ya hapa na pale katika baadhi ya maeneo hususan kaskazini mwa nchi hiyo, mapigano ambayo yalisabibisha askari wengi kuuawa. Mapigano hayo yaliyoyahusisha makundi ya wabeba silaha ambayo yalitia saini makubaliano ya amani yalishuhudiwa sana mjini Kidal, na weledi wengi wa mambo waliyataja kama tishio kubwa kwa juhudi za kurejesha amani nchini humo. Taarifa iliyotolewa na serikali ilizitaka pande husika kujizuia na kuhitimisha hali ya mchafukoge kwa kuzingatia maslahi ya wananchi. Wafuasi wa wanamgambo wanaobeba silaha wanaoiunga mkono serikali, wanawatuhumu waasi wa Harakati ya Azawad kuwa imeanzisha hujuma na kuvunja makubaliano ya usitishaji vita nchini. Siku iliyopita, waratibu wa maandamano ya mjini Bamako walitaka pia kulindwa mshikamano wa kitaifa kati ya wananchi hadi mwisho wa utekelezwaji wa makubaliano hayo ya amani.

Raia wa Mali wakiandamana katika mitaa ya Bamako

Maandamano hayo yamefanyika katika hali ambayo siku chache zilizopita kulifanyika kikao cha 10 cha kamati ya ufuatiliaji wa makubaliano ya amani nchini Mali, kikao ambacho kilimalizika kwa kufikiwa natija chanya. Kamati ya ufuatiliaji wa makubaliano ya amani inaundwa na wawakilishi wa serikali na makundi ya wabeba silaha, ambayo yanajitahidi kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa. Wajumbe wa kamati hiyo walipitisha uamuzi wa kuunda makundi ya kupiga doria kutoka pande zote mbili, yaani jeshi la serikali na makundi ya wabeba silaha yatakayokuwa na askari 600 kwa ajili ya kutembelea mji wa Gao kuanzia tarehe 15 ya mwezi ujao wa Agosti.

Maandamano ya wananchi nchini Mali jijini Bamako

Harakati ya Azawad ambayo ni miongoni mwa makundi ya wabeba silaha kaskazini mwa nchi, imeeleza matarajio yake ya kuwafungulia njia wanachama wake kwa ajili ya kurejea katika jamii. Kila yalipofikiwa makubaliano ya amani baina ya serikali na makundi ya wabeba silaha ya upinzani, kulikuwa kukijiri machafuko yaliyosababishwa na uvunjwaji wa makubaliano hayo, hata hivyo safari hii inaonekana kwamba pande husika zimeazimia kurejesha usalama nchini Mali sanjari na kutekeleza makubaliano. Hatua hizo zinajiri katika hali ambayo bunge limeongeza muda wa halli ya hatari nchini humo. Wabunge wote 99 waliohudhuria kikao cha jana Jumamosi wamepitisha kwa pamoja uamuzi wa kurefusha kipindi cha hali ya hatari kwa miezi minane mingine. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali ya hatari nchini Mali itaendelea hadi tarehe 29 mwezi Machi mwaka kesho 2017.

Mali hapo jana Jumamosi

Tangu mwaka jana serikali ya Bamako mbali na changamoto za makundi ya wabeba silaha kaskazini mwa nchi, imekuwa ikikabiliwa pia na mashambulizi ya kigaidi, suala lililoifanya serikali hiyo kutangaza hali ya hatari kuanzia tarehe 21 mwezi huu wa Julai.

Tags