Kenya yaiamuru TikTok iondoe maudhui za kingono zinazowalenga watoto
Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya imeutaka mtandao wa kijamii wa China wa TikTok uondoe maudhui za kingono zinazowalenga na kuwaathiri watoto.
Kwa mujibu wa taarifa ya kiuchunguzi iliyotolewa na mamlaka hiyo, jukwaa la TikTok lilikuwa likipata faida kutokana na maudhui hizo za mambo machafu zenye kuhusisha watoto wenye umri wa miaka 15.
Taarifa hiyo ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya imebainisha kuwa imeanza uchunguzi rasmi, huku ikisisitiza kwamba haitosita kuchukua hatua zozote stahiki dhidi ya mtandao huo wa nchini China.
Sheria za Kenya zinapiga marufuku udhalilishaji watoto kwa njia ya mtandao.
Itakumbukwa kuwa, siku ya Jumanne, raia wa Uholanzi alihukumiwa na mahakama ya Kenya kifungo cha miaka 10 jela kwa kusambaza picha za kingono za watoto kupitia mtandao wa WhatsApp.
Mtandao wa TikTok ndilo jukwaa la tatu kwa kuwa na wafuasi wengi duniani, likitanguliwa na Facebook na WhatsApp.
Mtandao huo uliwahi kuandamwa na shutuma za kufanya upelelezi nchini Marekani, na kwa sasa uko chini ya uchunguzi wa Umoja wa Ulaya kwa madai kwamba ulikuwa na ushawishi katika uchaguzi wa Rais wa Romania.../