Makumi ya Maelfu waandamana dhidi ya Rais Joseph Kabila
Makumi ya maelfu ya watu jana Jumapili waliandamana Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakipiga nara dhidi ya serikali na kuperurusha bendera za vyama vya upinzani. Wafanya maandamano wamemtaka Rais Joseph Kabila aondoke madarakani baada ya kumalizika muhula wake mwezi Novemba mwaka huu.
Kabila mwenye umri wa miaka 45 ambaye yupo madarakani huko Kongo tangu kuuliwa baba yake mwaka 2001, anakabiliwa na mashinikizo ya ndani na ya madola makubwa yanayomtaka aachie madaraka na kuitisha uchaguzi wa rais baada ya muhula wake kumalizika mwezi Novemba mwaka huu. Serikali ya Kinshasa imesema kuwa matatizo ya kilojistiki huenda yakachelewesha uchaguzi huku wafuasi wa Rais Kabila wakipendekeza kufanyika kura ya maoni ili kuondoa ukomo wa kipindi cha urais ili kumuwezesha rais huyo kugombea kwa mara nyingine kama walivyofanya viongozi wengine wa Kiafrika. Hata hivyo wapinzani Kongo wanasema kuwa Kabila anafanya kila mbinu ili kujaribu kusalia madarakani kwa kipindi kingine.
Maandamano ya jana katika mji mkuu Kinshasa yalifanyika kwa amani. Baadhi ya waandamanaji walinukuliwa wakisema kuwa watajaribu kumuondoa kwa nguvu madarakani Rais Kabila iwapo italazimu.