Wawakilishi wa Sudan na UAE walumbana katika mkutano wa Baraza la Usalama
(last modified Fri, 14 Mar 2025 13:02:08 GMT )
Mar 14, 2025 13:02 UTC
  • Al-Harith Idris
    Al-Harith Idris

Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York uliokuwa ukichunguza hali ya kibinadamu nchini Sudan umeambatana na malumbano na shutuma za pande mbili kati ya wawakilishi wa Sudan na UAE katika Umoja wa Mataifa.

Mkutano wa Baraza la Usalama wa jana Alkhamisi ulikuwa wa kwanza kufanyika baada ya Sudan kuiomba Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kufungua mashtaka dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kukiuka majukumu yake chini ya Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, ombi la Sudan linahusu hatua zilizofanywa na RSF na makundi washirika dhidi ya watu wa jamii ya Masalit nchini Sudan.

Akizungumzia matatizo ya wananchi wa Sudan, mwakilishi wa Imarati, Mohammed Abu Shihab amesema: "Uharibifu uko wazi kabisa na unatokana na uchaguzi mbaya wa majenerali wawili wanaozozana ambao wanang'angania vita bila kujali gharama zake kwa watu wa Sudan."

Akijibu matamshi ya mwakilishi wa Imarati, mwakilishi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Al-Harith Idris, ameituhumu Abu Dhabi kuwa inachochea moto wa vita nchini Sudan kwa lengo la kukalia kwa mabavu maeneo ya nchi hiyo na rasilimali zake kupitia njia ya kuwasaidia waasi wa RSF na akasema: "Suala hili pia limethibitishwa na ripoti ya wataalamu wa Baraza la Usalama la UN."

Baraza la Usalama la UN

Idris ameongeza kuwa: "UAE ina mchango mbaya na haribifu, na kama itaendelea kuwasaidia waasi  wa RSF matatizo yataendelea kuwepo."

Mwakilishi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa amesema: "Baraza la Usalama linapaswa kuitaja UAE badala ya kuzungumzia uingiliaji wa mawakala wa kigeni bila ya kutaja jina, na upande pekee wa kigeni anaoingilia vita nchini Sudan ni UAE."