MSF yatahadharisha kuhusu kasi kipindupindu Ethiopia; watu 31 wameaga dunia
Takriban watu 31 wapoteza maisha kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaoenea kwa kasi nchini Ethiopia.
Watu zaidi ya watu 1,500 katika eneo la Gambella nchini Ethiopia wameugua kipindupindu katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Taarifa hii imetolewa na Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF).
Jumuiya hiyo ya matibabu ya kimataifa imeeleza kuwa hali ya mambo inazidi kuwa mbaya katika eneo la Gambelle nchini Ethiopia kufuatia wimbi la watu wanaowasili katika eneo hilo wakikimbia mapigano katika nchi jirani ya Sudan Kusini.
MSF imesema ugonjwa wa kipindupindu unaenea kwa kasi kubwa magharibi mwa Sudan huku mlipuko huo ukiripotiwa pia huko Sudan Kusini na hivyo kuhatarisha maisha ya maelfu ya watu.
Majimbo kadhaa ya Ethiopia, nchi ya pili yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika ikiwa na watu milioni 120, yanapambana na milipuko ya kipindupindu, ambapo jimbo la Amhara - mbalo ni la pili kwa ukubwa huko Ethiopia, likiwa miongoni mwa majimbo yaliyoathiriwa zaidi na kipindupindu.
Kipindupindu ni ugonjwa hatari unaosababishwa na kumeza bakteria aitwaye Vibrio Cholerae. Dalili za kipindupindu zinazofahamika zaidi ni kuharisha sana na kutapika, ambazo zinaweza kusababisha upungufu mkubwa wa maji mwilini.
Kaunti ya Akobo katika eneo la Upper Nile huko Sudan Kusini, wiki nne zilizopita ilisajili wagonjwa 1,300 wa kipindupindu.