Mamia ya waasi wa Fano wauawa katika operesheni ya jeshi la Ethiopia
Wanajeshi wa Ethiopia wamewaua zaidi ya wapiganaji 300 wa kundi lenye silaha la Fano, washirika wao wa zamani dhidi ya waasi katika eneo la Tigray, katika siku mbili za mapigano mapya katika eneo la kaskazini la Amhara.
Jeshi la Ethiopia limesema katika taarifa kwamba, wapiganaji hao wa Fano walifanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya eneo la Amhara kabla ya "kuangamizwa" na jeshi katik operesheni ya kuwakabili na kuwarejesha nyuma.
Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, wapiganaji 317 wa kundi la waasi wa Fano waliuawa huku wengine 125 wakijeruhiwa katika operesheni hiyo.
Hata hivyo, Abebe Fantahun, msemaji wa Fano huko Wollo Bete-Amhara, amepinga idadi hiyo, na kuliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wapiganaji wao waliouawa hawafiki hata 30.

Naye Yohannes Nigusu, msemaji wa Fano huko Gondar, mkoa wa Amhara, amesema wanajeshi 602 wa jeshi la serikali waliuawa katika mapigano hayo na 430 kujeruhiwa, huku wanajeshi 98 wakikamatwa, mbali na silaha kutwaliwa na wapiganajiwa Fano.
Ikumbukwe kuwa, waasi wa Fano walipigana katika safu moja na jeshi la Ethiopia na vikosi vya Eritrea katika vita vya miaka miwili dhidi ya kundi la Tigray People's Liberation Front TPLF, ambalo linadhibiti eneo la kaskazini la Tigray.