Tunisia yalaaniwa kwa kumkamata mwanachuo aliyepeperusha bendera ya Palestina
(last modified Wed, 26 Mar 2025 11:12:10 GMT )
Mar 26, 2025 11:12 UTC
  • Tunisia yalaaniwa kwa kumkamata mwanachuo aliyepeperusha bendera ya Palestina

Mwanafunzi mmoja wa Tunisia amekamatwa kwa kuingia uwanjani na kupeperusha bendera ya Palestina wakati wa mechi ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tunis.

Katika taarifa yake, Muungano Mkuu wa Wanafunzi wa Tunisia (UGTE) umesema mwanafunzi huyo aliwekwa chini ya ulinzi baada ya kubomoa mabango yanayoiunga mkono Israel katika Uwanja wa Rades wakati wa mechi ya Jumatatu kati ya Tunisia na Malawi.

"Mwanafunzi huyo kisha alipeperusha bendera ya Palestina katika kuonyesha mshikamano na kadhia ya Palestina," imeongeza taarifa hiyo.

Muungano huo umelaani hatua ya kukamatwa mwanachuo huo na kuitaja kama "ukiukaji wa uhuru wa kujieleza na haki ya kuchukua msimamo thabiti na wazi kuhusu masuala ya kitaifa na kibinadamu."

Hali kadhalika Muungano Mkuu wa Wanafunzi wa Tunisia umesisitiza uungaji mkono wake kwa mikutano na mikusanyiko yote ya kuunga mkono kadhia ya Palestina.

Watunisia katika maandamano ya kuwatetea Wapalestina

Wananchi wa Tunisia walisambaza video kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu ikionesha kijana huyo akivamia Uwanja wa Rades, huku akipeperusha bendera ya Palestina na kuondoa nembo za biashara za Ufaransa zinazounga mkono Israel katika uwanja huo.

Tunisia imeshuhudia maandamano kadhaa ya kulaani vita vya mauaji ya halaiki vya Israel katika Ukanda wa Gaza, ambapo zaidi ya watu 50,100 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kikatili tangu Oktoba 2023.