Magaidi washambulia kambi za jeshi Nigeria, Cameroon na kuua askari 16
(last modified Thu, 27 Mar 2025 11:08:40 GMT )
Mar 27, 2025 11:08 UTC
  • Magaidi washambulia kambi za jeshi Nigeria, Cameroon na kuua askari 16

Watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa magenge ya kigaidi wamefanya mashambulizi yaliyoratibiwa dhidi ya kambi ya jeshi la Cameroon karibu na Ziwa Chad na dhidi ya kituo cha kijeshi kaskazini mashariki mwa Nigeria, na kuua takriban wanajeshi 16.

Duru za habari zimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa, katika shambulio la hivi punde zaidi, wapiganaji wa genge la kigaidi la Boko Haram na wale wa ISIS tawi la Afrika Magharibi ISWAP wameshambulia kambi ya jeshi katika eneo la Wajiroko katika Jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuteketeza vifaa vya kijeshi, mbali na kufanya mauaji.

Mmoja wa askari katika kikosi cha Wajiroko amesema takriban wanajeshi wanne wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa akiwemo kamanda wa kikosi hicho katika shambulio hilo la kigaidi.

Wakati huo huo, Wizara ya Ulinzi ya Cameroon imesema leo Alkhamisi kuwa, magaidi wenye silaha wakiwa na magari mepesi ya deraya pia walivamia kituo cha Wulgo, kijiji kilicho umbali wa kilomita 12 kutoka mji wa mpakani wa Cameroon wa Fotokol, karibu na Ziwa Chad na kuua wanajeshi 12 na kujeruhi wengine zaidi ya 10. 

Wanachama wa genge la kigaidi la ISWAP

Duru za habari zinasema kuwa, inashukiwa kuwa wanamgambo hao walianzisha mashambulizi yao kwa kutumia ndege zisizo na rubani kabla ya kuendelea na mashambulizi ya ardhini. "Walipora akiba muhimu ya silaha," chanzo kimoja kimesema.

Wanamgambo wa Boko Haram na ISWAP wamekuwa wakiendesha shughuli zao kaskazini mashariki mwa Nigeria, wakishambulia vikosi vya usalama na raia na kuua na kuwafurusha makumi ya maelfu ya watu.

Jeshi la Nigeria halijatoa taarifa yoyote kuhusiana na hujuma hizo. Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Cameroon, Cyrille Serge Atonfack Guemo amethibitisha habari ya kutokea shambulio hilo lakini amesema idadi ya waliouawa na kujeruhiwa bado haijafahamika.