Waziri: Makubaliano ya amani Sudan Kusini yamevunjika
Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan Kusini umechukua mwelekea mpya baada ya Waziri wa Kilimo wa nchi hiyo kutoka upande wa upinzani kujiuzulu na kusisitiza kuwa makubaliaono ya amani yaliyosainiwa na pande mbili yamevunjika.
Dakta Lam Akol ambaye pia ni kinara wa chama upinzani cha SPLM-DC ametangaza kujiuzulu huku akimtaka Rais Salva Kiir kufuata mkondo huo na kuvunja serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo. Kadhalika Dakta Akol amemshambulia kinara wa upinzani na Makamu wa Kwanza wa Rais aliyeiotoroka Juba, Riek Machar, ambaye wanajeshi wake wamekuwa wakikabiliana na askari wanaomuunga mkono Kiir katika mji mkuu Juba. Machafuko mapya mjini Juba yamepelekea kuuawa watu wasiopungua 300 hadi sasa na kutishia kuzuka tena vita vya ndani huko Sudan Kusini.
Hii ni katika hali ambayo, James Wani Igga, Makamu wa Pili wa Rais wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika hivi karibuni alisema Rais Salva Kiir amemteua Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais aliyejaza nafasi ya Machar kuongoza ujumbe wa upinzani kwenda mjini New York makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuushawishi umoja huo uunge mkono serikali ya sasa inayoongozwa na yeye na Kiir. Baadaye Deng Gai anatazamiwa kuelekea Khartoum nchini Sudan kukutana na viongozi wa jumuiya ya kieneo ya IGAD kujadili suala hilo la uongozi mpya.
Hii ni licha ya kuwa Riek Machar anasisitiza kuwa angali Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hiyo na kwamba karibuni hivi atarejea mjini Juba kuendelea kushikilia wadhifa wake.