Aug 02, 2016 07:57 UTC
  • Waasi wa FLEC wadai kuua askari 17 wa jeshi la Angola

Waasi wa kundi linalopigania kujitenga eneo la Cabinda nchini Angola FLEC wamedai kwamba wameua askari 17 wa nchi hiyo katika makabiliano makali yaliyojiri mwishoni mwa wiki iliyomalizika.

Kundi hilo linadai kwamba liliua papo hapo askari 11 wa Angola katika makabiliano ya Jumamosi jioni karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwamba 6 wengine waliuawa baada ya waasi hao kuliteka gari la jeshi hilo.

Jose Eduardo dos Santos, Rais wa Angola

Duru za kijeshi zimeliarifu shirika la habari la AFP kuwa ni kweli makabiliano hayo yalijiri lakini hazijatoa takwimu za waliouawa au kujeruhiwa katika mkoa wa Cabinda, ulioko umbali wa kilomita 380 kaskazini mwa mji mkuu wa Angola, Luanda na hauna mpaka wa pamoja na Angola.

Mwezi Machi mwaka huu 2016, kundi hilo la waasi lilidai kuwa limeua askari 30 wa Angola kwa kuwafyatulia risasi katika eneo hilo.

Ramani ya Angola

Kundi hilo ni moja ya makundi matatu ya wapiganaji wa msituni ambayo yanapigania kujitenga kwa jimbo lenye utajiri wa mafuta la Cabinda kutoka serikali kuu ya Angola. Jimbo la Cabinda ambalo kijiografia limejitenga na Angola, liko kati ya mpaka wa Congo Brazaville na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Jimbo hilo lina wakazi wapatao laki nne.

Tags