Makumi ya wanajeshi na raia wauawa katika shambulizi mashariki mwa Burkina Faso
Makumi ya wanajeshi na raia kutoka makundi yanayoliunga mkono jeshi la Burkina Faso wameuawa katika shambulio linaloshukiwa kufanywa na makundi yenye silaha mashariki mwa nchi hiyo.
Duru za ndani na za usalama zimeliambia shirika la habari la AFP kwamba "mashambulizi hayo makali yalilenga kikosi cha Diapaga," mji mkubwa zaidi katika mkoa wa Tapoa mashariki mwa Burkina Faso, na kuua makumi ya watu samabamba na kujeruhi idadi kubwa ya wengine. Chanzo hicho kimeeleza kuwa wahanga wa mashambulizi hayo ni "askari na raia wa kujitolea wanaolisaidia jeshi la taifa."
Chanzo kingine cha usalama kimethibitisha shambulio hilo lililotokea Ijumaa iliyopita, kikieleza kwamba "magaidi kadhaa waliangamizwa katika operesheni kubwa ya kulisafisha eneo hilo."
Tangu 2015, Burkina Faso imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya makundi yenye silaha yanayohusishwa na al-Qaida na ISIS. Mashambulizi haya yameua zaidi ya watu 26,000 na kuwalazimisha wengine milioni mbili kuwa wakimbizi.