Ukatili wa Polisi Dhidi ya Waandamanaji wa Siku ya Kimataifa Quds Nchini Nigeria
Katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds yaliyofanyika nchini Nigeria Ijumaa kwa kushirikisha mamia ya Waislamu na wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo – kwa lengo la kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina na kulaani uhalifu wa utawala wa Kizayuni wa Israel– maafisa wa polisi wa Nigeria walifyatua risasi dhidi ya waandamanaji. Tukio hilo lilisababisha waandamanaji wasiopungua 18 kuuawa shahidi, wengine kujeruhiwa, na wengi kukamatwa.
Sheikh Sidi Munir, mmoja wa viongozi waandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, amelaumu jeshi la Nigeria kwa tukio hilo na kusema: “Haya yalikuwa maandamano ya amani, lakini kwa bahati mbaya, kutokana na mashambulizi ya vikosi vya usalama, baadhi ya waandamanaji waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa.”
Isa Sanusi, Mkurugenzi wa Amnesty International tawi la Nigeria, ametaka kufanyika kwa uchunguzi huru na wa haki kuhusu mapigano ya umwagaji damu yaliyotokea Siku ya Kimataifa Quds. Amesema: “Jeshi lilitumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji, jambo linaloashiria kuwa huwa wanawalenga Waislamu waandamanaji kwa nia ya kuwaua.”
Hili si tukio la kwanza kwa jeshi la Nigeria kufyatua risasi dhidi ya Waislamu wanaoshiriki maandamano. Mnamo mwaka 2015, mashambulizi ya vikosi vya usalama dhidi ya Waislamu waliokuwa kwenye maombolezo ya Ashura katika mji wa Zaria yalipelekea vifo na majeraha kwa mamia, huku kiongozi wa Harakati ya Kiislamu, Sheikh Ibrahim Zakzaky, na mkewe wakikamatwa. Mashambulizi hayo yamekuwa yakiendelea kwa miaka iliyofuata, ambapo Waislamu – hasa Waislamu wa madhehebu ya Shia – waliokuwa wanaohiriki ibada na maandamano wamekuwa wakikumbwa na ukandamizaji na mateso kutoka kwa vyombo vya usalama.
Ingawa maafisa wa serikali ya Nigeria walitarajia kuwa kwa kuwakandamiza na kuwaongezea mashinikizo Waislamu wangeacha kushiriki katika matukio ya kidini kama Ashura, Taasua na Siku ya Quds, bado Waislamu wa Nigeria wameendelea kushiriki kwa wingi. Hali hii imepelekea vyombo vya usalama vya nchi hiyo kukabiliana na mikusanyiko yoyote ya Waislamu kwa ukatili mkubwa.
Mwaka huu pia, kutokana na uhalifu unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Waislamu wa Gaza na hali ngumu ya Wapalestina, Waislamu duniani kote waliandamana kwa wingi katika Siku ya Quds, hali ambayo nchini Nigeria ilisababisha makabiliano na kupelekea baadhi ya washiriki kuuawa shahidi tena.

Baraza la Uratibu wa Tablighi ya Kiislamu la Iran limetoa taarifa ya kulaani ukandamizaji waliofanyiwa Waislamu wa Nigeria wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds na kuandika: "Ukandamizaji na kumwagwa damu za waandamanaji wa Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Nigeria na kuuawa shahidi kidhulma Waislamu 18 waliokuwa kwenye saumu ya Ramadhani kunaonesha hofu ya watawala wa Nigeria kuhusu mwamko wa Waislamuj na nafasi ya kiistratijia ya Siku ya Kimataifa ya Quds duniani."
Sababu za kuongezeka kwa sera kali za serikali ya Nigeria dhidi ya Waislamu zinaweza kuhusishwa na mabadiliko ya kisiasa ya ndani, hali ya kimataifa, ongezeko la uingiliaji wa madola ya kigeni, utajiri mkubwa wa nishati, pamoja na nafasi ya Nigeria kama nchi kubwa zaidi na yenye Waislamu wengi zaidi barani Afrika. Kwa miaka ya hivi karibuni, serikali ya Nigeria imechukua mtazamo wa kiusalama dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. Ushawishi wa utawala haramu wa Israel na washirika wake nchini humo, na mashinikizo yao kwa serikali, kumechangia katika kuongeza mateso dhidi ya Waislamu wa Nigeria.
Kwa mujibu wa Shaibu Musa, mmoja wa wahadhiri wa vyuo vikuu nchini Nigeria, Marekani na washirika wake wanajaribu kuvunja uhuru wa kidini ulioainishwa katika katiba ya Nigeria na kuchochea mgawanyiko wa kidini na kimadhehebu. Amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, hali hii imekuwa dhahiri kupitia mashambulizi ya moja kwa moja ya vikosi vya usalama dhidi ya Waislamu.
Katika Siku ya Quds pia, maandamano ya Waislamu wa Nigeria na tamko lao la mshikamano na Wapalestina pamoja na kulaani uvamizi wa Israel dhidi ya Waislamu wa Gaza yaliamsha hasira ya baadhi ya maafisa wa serikali, na kusababisha jeshi kufyatua risasi dhidi ya waandamanaji.
Licha ya shinikizo zote hizi, Waislamu wa Nigeria bado wameshikamana na misingi ya Kiislamu na wanaendelea na harakati zao. Katika hilo, Sheikh Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, amesema hivi karibuni:
“Baada ya kumwagika kwa damu nyingi kiasi hiki, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, Gaza itashinda, na kisha Palestina itashinda, na hivi karibuni tutaswali pamoja katika Msikiti wa Al-Aqsa.”