Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Burkina Faso na Niger kukutana mjini Moscow wiki hii
(last modified Wed, 02 Apr 2025 07:03:33 GMT )
Apr 02, 2025 07:03 UTC
  • Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Burkina Faso na Niger kukutana mjini Moscow wiki hii

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Burkina Faso na Niger wiki hii wataelekea ziarani mjini Moscow, Russia. Nchi hizo za eneo la Sahel barani Afrika zinaizuru Moscow katika jitihada za kuimarisha uhusiano wao na Russia.

Serikali za Mali, Burkina Faso na Mali ambazo zinaongozwa na viongozi wa kijeshi na ziliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi ya miaka ya karibuni, zimeunda muungano wa Confederation of Sahel States (AES) au Shirikisho la Nchi za Sahel. 

Muungano huo wa nchi tatu za Magharibi mwa Afrika umefukuza katika nchi hizo vikosi vya majeshi ya Ufaransa na nchi  nyingine za Magharibi na kisha kuigeukia Russia kwa ajili ya msaada wa kijeshi.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo tatu wataitembelea Moscow Alhamisi na Ijumaa wiki hii na kufanya mazungumzo na waziri mwenzao wa Russia, Sergei Lavrov. 

Wamesema "mkutano wa Moscow ni hatua muhimu katika kuanzisha ushirikiano wa kimkakati, kivitendo, wenye nguvu na ushirikiano katika maeneo yenye maslahi ya pamoja kati ya Shirikisho la Nchi za Sahel na Russia."