Sudan yaiambia ICJ kuwa UAE inachochea mauaji ya halaiki Darfur
(last modified Fri, 11 Apr 2025 02:06:27 GMT )
Apr 11, 2025 02:06 UTC
  • Sudan yaiambia ICJ kuwa UAE inachochea mauaji ya halaiki Darfur

Sudan iliiambia Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) jana Alhamisi kwamba, Umoja wa Falme za Kiarabu umekiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari kwa kuunga mkono vikosi vya wanamgambo huko Darfur, na kuwataka majaji wa mahakama hiyo kutoa amri ya dharura ya kuzuia mauaji ya kimbari katika eneo hilo.

Malalamiko ya Sudan kwa ICJ yenye makao yake mjini The Hague yanahusiana na mashambulizi makali ya kikabila yaliyofanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na wanamgambo washirika wa Kiarabu dhidi ya kabila lisilo la Kiarabu la Masalit mnamo 2023 huko Darfur Magharibi. Khartoum inaituhumu Abu Dhabi kuwa imekiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari kwa kuwapa silaha na kuwafadhili kifedha wanamgambo wa RSF katika vita vya ndani vya Sudan.

"Mauaji ya halaiki dhidi ya Masalit yanatekelezwa na Kikosi cha RSF kinachoaminika kuwa cha Waarabu kutoka Darfur, kwa msaada na ushirikiano wa Umoja wa Falme za Kiarabu," Kaimu Waziri wa Sheria wa Sudan, Muawia Osman, ameiambia ICJ.

Sudan imedai katika mashtaka yake kwamba UAE ilihusika na mauaji hayo ya kimbari ya Wasudan wa kabila la Masalit "kwa kuelekeza na kutoa msaada mkubwa wa kifedha, kisiasa na kijeshi kwa wanamgambo wa RSF.

Athari za mapigano Darfur Magharibi

Kwa upande wake, Umoja wa wa Falme za Kiarabu, umeiambia mahakama hiyo kwamba, madai yaliyotolewa katika kesi ya Khartoum "hayana msingi wa kisheria au wa kweli" na kwamba kesi hiyo ni jaribio la kuondoa mazingatio ya fikra za umma kuhusiana na vita vya maafa makubwa vinavyoendelea nchini Sudan. Abu Dhabi inataka Mahakama ya Kimataifa ya Haki itupilie mbali mara moja kesi hiyo ikisisitiza kuwa haina msingi.

"Hakukuwa na ushahidi wa kuaminika uliowasilishwa kuyapa nguvu madai (ya Sudan)," Reem Ketait, afisa wa ngazi ya juu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE amesema katika taarifa baada ya Sudan kuwasilisha kesi hiyo mbele ya ICJ.

Kwa kuwa kesi katika mahakama ya ICJ huchukua miaka kadhaa kabla ya kutolewa uamuzi wa mwisho, mataifa yanaweza kuomba hatua za dharura ambazo zinakusudiwa kuhakikisha mzozo kati ya majimbo husika hauongezeki kwa sasa.