Mamia wauawa na kujeruhiwa katika shambulio la RSF kwenye kambi ya Zamzam
-
El Fasher, Darfur Kaskazini
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan na mashirika ya misaada ya kibinadamu yamesema kuwa mamia ya watu wameuawa na kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa jana na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwenye kambi ya Zamzam ya wakimbizi wa ndani katika mji wa El Fasher, Jimbo la Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan.
Uratibu Mkuu wa Watu Waliogura Makazi na Wakimbizi umesema katika taarifa kwamba wimbi la kwanza la mashambulizi lilianza siku ya Alkhamisi na kuendelea hadi Ijumaa na Jumamosi, na kuharibu nyumba, masoko na vituo vya afya.
Kamati ya uratibu imesema mashambulizi hayo "yameua na kujeruhi mamia ya watu, ambao wengi wao walikuwa wanawake na watoto." Kamati ya Uratibu imelaani mashambulizi hayo, ikiyataja kuwa ni "uhalifu kamili wa kivita na jinai dhidi ya ubinadamu."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mashambulizi kama hayo kwenye kambi ya Abu Shouk wiki iliyopita yalisababisha vifo vya raia 35.
"Hali ya kibinadamu huko El Fasher inaporomoka kwa kasi kuelekea kwenye janga ambalo halijawahi kutokea," imesema taarifa hiyo, ikiashiria njaa, uhaba wa dawa na ukosefu kamili wa usalama katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Gavana wa Jimbo la Darfur Kaskazini Al-Hafiz Bakhit amesema kuwa Vikosi vya Msaada wa Haraka vimeua makumi ya Wahifadhi Qur'ani katika kituo cha Sheikh Farah katika kambi ya Zamzam, sanjari na kulengwa kwa silaha nzito kambi ya Abu Shouk, na kusababisha vifo na majeruhi.
El Fasher ni kitovu kikuu cha operesheni za misaada ya kibinadamu huko Darfur na imekuwa ikishuhudia mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka tangu Mei 10, 2024, licha ya onyo kuhusu kimataifa la hali mbaya ya binadamu katika eneo hilo.