Kamanda wa kikosi cha kupambana na Boko Haram ataka wananchi watoe ushirikiano
Kamanda wa kikosi cha mataifa kadhaa kinachoendesha operesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram amewataka wakazi wa maeneo ya mipaka ya Nigeria, Niger, Chad na Cameroon kutoa ushirikiano kwa vikosi hivyo kwa ajili ya kupambana na wanamgambo hao.
Meja Jenerali Lamidi Adeosun amesema hayo katika mji mkuu wa Niger Niamey na kubainisha kwamba, kuna haja kwa wakazi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa kikosi hicho ili kifanikiwe katika operesheni zake za kijeshi dhidi ya Boko Haram.
Meja Jenerali Adeosun amesema kuwa, wakazi wa maeneo hayo wanapaswa kuwasilisha taarifa kwa vikosi hivyo kuhusiana na ingia toka ya raia wa kigeni katika maeneo hayo.
Aidha Kamanda wa kikosi cha mataifa kadhaa kinachoendesha operesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram amesisitiza kuwa, operesheni za vikosi hivyo zitaendelea hadi pale watakapofanikiwa kung'oa kabisa mizizi ya kundi hilo la kigaidi.
Hivi karibuni, Jeffrey Feltman afisa wa ngazi za juu katika Umoja wa Mataifa alisema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, kikosi kilichoundwa na Nigeria, Chad, Cameroon, Niger na Benin kwa ajili ya kupambana na kundi la Boko Haram kimefanikiwa kuwafurusha wanamgambo wa kundi hilo katika maeneo mengi.
Hata hivyo akasema nchi za eneo la Ziwa Chad zinahitaji kuungwa mkono ipasavyo na jamii ya kimataifa ili kuweza kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo na vilevile kufanikisha vita dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram.
Ripoti zinaonesha kuwa, kikosi hicho hadi sasa kimefanikiwa kukomboa asilimia 80 ya maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na kundi la Boko Haram, kuokoa maelfu ya watu waliokuwa wametekwa nyara na kundi hilo na kuzuia mashambulio kadhaa ya kigaidi.