Rais wa Burundi azindua kampeni ya uchaguzi wa 2025 wa wabunge na wilaya
(last modified Sat, 10 May 2025 06:54:41 GMT )
May 10, 2025 06:54 UTC
  • Rais wa Burundi azindua kampeni ya uchaguzi wa 2025 wa wabunge na wilaya

Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi jana Ijumaa alizindua rasmi kampeni ya uchaguzi wa pamoja wa wabunge na wilaya, unaotarajiwa kufanyika Juni 5, akiwa Gitega, mji mkuu wa kisiasa wa nchi hiyo.

Ikiwa ni mara ya kwanza kwa Burundi, uzinduzi huo umehusisha gwaride la karibu wagombea 10,000 watakaoshiriki uchaguzi ujao wa Juni 2025. Washiriki walivaa sare za vyama vyao vya siasa na kuonyesha alama watakazotumia wakati wa kampeni za wiki tatu za uchaguzi, zitakazoanza Mei 13 hadi Juni 2.

Akihutubia mkutano huo, Ndayishimiye amewataka wagombea kutangaza sera na ilani zenye uhalisia na zenye manufaa na sio kutoa ahadi hewa.

"Kuona wagombea wote kwenye uchaguzi wakishiriki kikamilifu ni tukio maalumu la kipekee katika historia ya Burundi. Hii ni hatua kubwa katika demokrasia na umoja wa Burundi," amesema.

"Tukio hili ni ushahidi wa kweli kwamba uchaguzi ni mchezo tu ambao mwisho wake mshindi anakubali uungaji mkono wa aliyemshinda," amesema na kusisitiza kwa kusema, inabidi kujiepusha na vita, isije ikawa kama ilivyotokea huko nyuma nchini Burundi.

Katika agizo la rais alilotoa jana Ijumaa, Ndayishimiye ametangaza saa za kampeni kuwa ni kutoka 12 asubuhi hadi 12 jioni, kwa majira ya ndani ya Burundi. Amewataka wagombea kuepuka kufanya mikutano katika maeneo ya kazi na kuomba vibali vya kufanya kampeni zao.

Mbali na uchaguzi wa wabunge na wilaya wa Juni 5, Burundi itaandaa uchaguzi wa maseneta Julai 23 na uchaguzi wa ngazi ya vijiji Agosti 25 mwaka huu. Uchaguzi ujao wa rais utafanyika mwaka 2027.