Waliokufa kwenye mafuriko DRC wafika 62 na 50 hawajulikani walipo
Takriban watu 62 wamethibitishwa kufariki dunia na wengine 50 hawajulikani walipo baada ya mafuriko makubwa kuvikumba vijiji vilivyoko karibu na Ziwa Tanganyika katika jimbo la Kivu Kusini, huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Watu walioshuhudia wamesema kuwa, mafuriko hayo yalianza yapata saa piga mwendo wa saa 11 alfajiri kwa majira ya mashariki mwa DRC wakati maji ya mafuriko yalipokumba kijiji cha Kasaba cha kata ya Ngandja. Wenyeji wa maeneo hayo wamesema kuwa mvua kubwa imesababisha mafuriko, kusomba nyumba na kukata mawasiliano.
Waziri wa afya wa jimbo la Kivu Kusini, Theophile Walulika Muzaliwa amesema kwamba juhudi za kutafuta watu zaidi na kuokoa kinachowezekana zimekwamishwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na miundombinu duni.
Wakuu wa maeneo hayo wakiwemo machifu wa vijiji na wakuu wa serikali za mitaa, wamethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, shirika pekee la misaada ya kibinadamu lililopo kwenye eneo hilo hadi wakati inaripotiwa habari hii, lilikuwa ni la Msalaba Mwekundu. Waziri Muzaliwa amesema kuwa, haiwezekani kutoa tathmini yoyote kwa sasa kwani zoezi la uokoaji bado linaendelea.
Mafuriko hayo yametokea wiki kadhaa baada ya mvua kama hiyo kuua watu 33 katika mji mkuu Kinshasa. Miundombinu yote ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeathiriwa na mafuriko na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika miezi ya hivi karibuni.
Mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi yenye silaha yaliongezeka mwezi Februari na kuzidisha kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita kuwa ni moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.