Aug 05, 2016 04:52 UTC
  • Uganda yaahidi kuisaidia DRC kupambana na waasi wa ADF

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameahidi kuwa serikali yake itaisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kukabiliana na kundi la waasi la ADF-Nalu ambalo limekuwa tishio la muda mrefu la nchi mbili hizo jirani.

Rais Museveni aliyasema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake na Rais Joseph Kabila wa Kongo DR katika kituo cha mpakani cha Mpondwe mjini Bwera wilaya ya Kasese. Rais Museveni amesema yuko tayari kutuma askari wa jeshi la UPDF kwenda kuzima harakati za kundi hilo haswa mashariki mwa DRC.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Mapema mwezi jana, watu 9 waliuawa na kundi la waasi wa ADF-Nalu wa Uganda katika kijiji cha Oicha kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Waasi wa ADF

Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, Rais Museveni akizungumza katika dhifa ya chakula cha futari katika Ikulu ya Entebbe, alisema tayari amemuandikia barua Rais Joseph Kabila wa Kongo DR akimtaka alishugulikie suala hilo na kusisitiza kuwa, waasi wa ADF-Nalu wamekuwa wakivizia na kuwaua wasomi wa Kiislamu nchini Uganda na kisha kurejea mafichoni katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekuwa likishuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa kutokana na kuwa ngome ya makundi kadhaa ya waasi kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda. Baadhi ya vijiji vya mashariki mwa nchi hiyo vinadhibitiwa na makundi ya waasi hali ambayo imewafanya wakazi wake kuyaacha makazi yao na kuwa wakimbizi.

Tags