Rais Traoré wa Burkina Faso aikosoa vikali kamandi ya kijeshi ya Marekani barani Afrika
Rais Ibrahim Traoré wa Burkina Faso amemkosoa vikali mkuu wa Kamandi ya Kijeshi ya Marekani barani Afrika kwa kuingilia mambo ya ndani ya nchi yake huku akisema kuwa Muungano wa Nchi za Sahel ulioundwa hivi karibuni ni “Mfano wa Mshikamano” barani Afrika.
Traoré ambaye alitembelea mji mkuu wa Russia, Moscow, kusherehekea miaka 80 ya ushindi wa Umoja wa Kisovieti dhidi ya Ujerumani ya Nazi katika Sherehe za Ushindi, alitoa maoni hayo katika mahojiano na Sputnik News. Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) ulioundwa na Mali, Niger na Burkina Faso mwaka 2023, umebadili kabisa mlingano wa nguvu za kimkakati kwa madola ya kikoloni ambayo yanataka kuendelea kutawala nchi hizo. Muungano huo unafanya mabadiliko makubwa ya kistratejia ya kimataifa, ikiwemo kujiondoa kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS)
Katika mahojiano hayo Rais Traoré amekosoa jumuiya kiuchumi wa Afrika Magharibi, ECOWAS, akilaumu shirika hilo la kikanda kwa kudanganya nchi ambazo ilikuwa imeahidi kuzisaidia. Traoré amesema vikwazo kutoka ECOWAS vimevuruga nchi za Sahel badala ya kuimarisha mshikamano:
Rais Traoré amelaani kuundwa kwa kikosi cha kijeshi kilichokusudiwa kupambana na nchi za Muungano wa Mataifa ya Sahel badala ya kuziunga mkono dhidi ya tishio la pamoja la ugaidi. Traoré ameongeza kuwa: “Wananchi, hata katika nchi hizi za ECOWAS, wanaiunga mkono na wanaelewa malengo ya Muungano wa Mataifa ya Sahel.”
Traoré, ambaye amelinganishwa na kiongozi wa mapinduzi wa Burkina Faso, Thomas Sankara, alifichua gharama binafsi ya uongozi wake. Katika juhudi zake za kufikia Umajumui wa Afrika, amejitolea usingizi wake. Amesema “Nilikuwa ninalala masaa mawili, sasa nimepunguza hadi saa moja.”
Amesema ataendelea kuwa mwaminifu katika mapambano ya Umajumui wa Afrika, vita anavyoona kuwa muhimu kwa uhuru kamili wa bara Afrika.
Kiongozi huyo mashuhuri wa Burkina Faso amesema: “Afrika imeteseka sana. Ni wakati wetu kuungana, kufanya kazi, kujiendeleza. Ni jukumu letu na tutalitekeleza!”

Nguzo kuu ya maono yake ya uhuru ni jeshi lenye nguvu na linalojitegemea. Traoré amelalamika jinsi vikosi vya kigeni vilivyodhoofisha uwezo wa ulinzi wa taifa la Burkina Faso. Traoré ameikosia vikali AFRICOM, Kamandi ya Kijeshi ya Marekani barani Afrika, akilaumu makamanda wa kikosi hicho kwa kwa kueneza uongo kuhusu ushirikiano wa kimataifa wa Burkina Faso na usimamizi wa akiba ya dhahabu ya nchi hiyo. Amesema “Tunayo haki ya kuanzisha uhusiano na yoyote tunayemtaka, huu ndiyo uhuru." Amemtaka kamanda AFRICOM kufuta taarifa zake potofu na kuomba radhi.
Hivi karibuni Kamanda wa AFRICOM, Michael Langley, alitoa ushahidi mbele ya Kamati ya Huduma za Kijeshi ya Bunge la Seneti la Marekani na kumtuhumu Traoré, kwa kutumia akiba ya dhahabu ya Burkina Faso aliyoitaifisha ili “kulinda utawala wake wa kijeshi.”
Akimjibu kamanda huyo wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Traoré amesema, “Anapaswa kujitazama kwenye kioo, aone aibu, na atoke hadharani aseme, ‘Nilipatiwa taarifa zisizo sahihi. Najutia hilo."