Mali yatengua vyama vyote vya siasa na 'mashirika'
Serikali ya kijeshi nchini Mali inayoogozwa na Jenerali Assimi Goita imetangaza kusitisha shughuli za vyama vyote vya kisiasa na mashirika ya kiraia 'yenye muundo wa kisiasa' katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Waziri anayehusika na mageuzi ya serikali, Mamani Nassire, ametangaza uamuzi huo kupitia taarifa iliyotolewa kupitia televisheni ya taifa wakati wa mkutano maalum wa Baraza la Mawaziri. Katika wiki za hivi karibuni, kumekuwepo na jaribio la mara kwa mara la kupinga kusitishwa kwa shughuli za vyama vya kisiasa nchini humo.
Mwezi uliopita April mwaka huu, mawaziri wa Mali walipendekeza kuongezwa muda wa kuhudumu kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo, Assimi Goita hadi mwaka 2030.
Goita ambaye aliingia madarakani kupitia mapinduzi mawili ya kijeshi mwaka 2020 na 2021, ameahidi kuandaa uchaguzi, japo mipango hiyo imeahirishwa kwa “sababu za kiufundi” bila ya kutolewa muda maalum wa kufanyika kwa zoezi hilo.
Kwa mujibu wa tangazo hilo la Mamani, watu wanaohudumu katika taasisi za kisiasa na kiutawala za serikali kwa sababu ya kuteuliwa kisiasa wanaweza kuendelea na majukumu yao, lakini bila kudai kuwa ni sehemu ya chama chao.
Serikali ya mpito inabainisha kuwa hatua hii inafuatia kufutwa kwa mkataba wa vyama vya siasa. “Tuko katika mchakato wa mageuzi,” ameeleza Mamani Nassiré, akibainisha kuwa mchakato huo utaendelea. Itabidi sheria mpya itungwe hasa kwa ajili ya usimamizi wa maisha ya kisiasa ya Mali.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeukosoa uamuzi huo, likidai kuwa eti ni pigo jingine kwa demokrasia nchini Mali.