Kiongozi Muadhamu: Iran ina wajibu wa kusimama dhidi ya tawala kandamizi
(last modified Thu, 15 May 2025 04:40:19 GMT )
May 15, 2025 04:40 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Iran ina wajibu wa kusimama dhidi ya tawala kandamizi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema lazima Iran isimame dhidi ya tawala zinazoua watoto pamoja na wale wanaowaunga mkono na kusitisha ukandamizaji, na itaendelea kufanya hivyo licha ya uadui unaoibuliwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, katika hotuba aliyotoa kwa wafanyakazi wa kutoa misaada wa Iran siku ya Jumatatu, aliwafananisha wanajeshi wa Israeli huko Gaza na “wanyama wakali waliovaa sura ya binadamu wanaopiga mabomu magari ya wagonjwa, hospitali, wagonjwa na kuwaua watoto wasio na hatia kwa ukatili wa hali ya juu.”

Ameendelea kuhoji: “Nani anaweza kudai na kuamini kwa dhati, kwamba mbele ya ukatili huu, mbele ya kiu  hiki cha damu, mwanadamu hana wajibu wowote? Nani anaweza kusema hivyo? Sote tuna jukumu.”

Kiongozi Muadhamu aidha amesema kuwa tawala hizi za kinyonyaji kwa sasa ndizo zinazotawala dunia, na kwamba Iran inazikabili ili kubadilisha hali ya sasa ya mambo duniani.

Ayatullah Khamenei amesema:  “Harakati ya Jamhuri ya Kiislamu, kusimama imara kwa Jamhuri ya Kiislamu, na ‘ustaarabu mpya’ ambao Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikiuashiria mara kwa mara, vyote vinaelekezwa katika kukabiliana na hali hii ya dunia."

Kiongozi Muadhamu amebainisha kuwa muqawama na kusimama kidete Iran dhidi ya dhulma ndio chanzo cha uhasama wa baadhi ya mataifa ya Magharibi dhidi ya nchi hii.

Amesema: “Ni hisia hii ya kuwajibika ndiyo inawapelekea maadui kama hawa makatili wa Magharibi, wanaojitokeza kwa dhahiri ya mavazi mazuri, na wakiwa wamepaka marashi, na wanaonekana wema, kusimama kwa uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.”

Aidha amesema:  “Ukikaa kimya mbele ya matendo haya ya kinyama, ukayakubali au hata kuyasifu, hawatakuwa na uadui wowote na wewe. Tatizo ni kuwa tunakataa msingi wa ustaarabu huu wa uongo, na tuko sahihi katika msimamo huu; ni lazima tukatae (uongo huo)."

Ayatullah Khamenei amesema kuwa dunia inaweza kuushinda uongo huu kwa hatua na msimamo thabiti.

“Ukisimama kidete bila shaka yoyote, wao watarudi nyuma. Lakini ukikaa kimya, ukaonyesha uso wa urafiki, ukatabasamu, ukakimbia au hata kuwasifia, la hasha, hawatatoweka; bali watakuwa na ukatili zaidi kila siku.”